[go: up one dir, main page]

Nenda kwa yaliyomo

Uinjilishaji

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru


Uinjilishaji (kutoka neno Injili) ni msamiati wa teolojia ya Kikristo ambao unajumlisha kazi mbili tofauti: kutangaza Injili kwa wasio Wakristo ili wamuamini Yesu Kristo[1], na kurekebisha jamii nzima ili isiishi kinyume na maadili yanayodaiwa na Mungu bali imani ipenye utamaduni wa waumini na kwa njia yao ule wa umati[2]. Ndiyo sababu hauishii katika kutangaza mbiu ya kwanza bali inaendelea katika katekesi na malezi kwa jumla, kwa mfano katika shule za Kanisa.

Katika Biblia

[hariri | hariri chanzo]

Neno la Kigiriki euangelion (lilitoholewa na Waarabu kama "Injil") na yale yanayotokana nalo kwa jumla yanapatikana mara 76 katika Agano Jipya (56 katika nyaraka za Mtume Paulo, 12 katika vitabu vya Injili, hasa Marko, lakini pia Mathayo). Linatumika daima katika uhusiano na Yesu, ujumbe wake, ufufuko wake na ujio wake wa pili.

Historia ya uinjilishaji

[hariri | hariri chanzo]

Kwa Mathayo na Marko, Yesu aliinjilisha. Lakini ni hasa Kanisa ambalo kuanzia Pentekoste linapaswa kuinjilisha kwa uwezo wa Roho Mtakatifu likimtangaza Yesu Kristo kuwa Bwana. Mwaka uleule wa kifo chake (30 kama si 33), katika siku hiyo Mitume wa Yesu walimtangaza kwa Wayahudi na wengineo wa lugha mbalimbali waliokuwa wamekusanyika Yerusalemu kwa ajili ya sherehe hiyo.

Uinjilishaji uliendelea kwa juhudi za watu kama wainjilisti Stefano na Filipo, mitume Barnaba e Paolo waliozidi kwenda mbali wakihubiri kwanza kwa Wayahudi lakini pia kwa mataifa yote. Kilichosaidia sana wongofu wa wengi kati ya hao wa pili ni mtaguso wa Yerusalemu (49 hivi), ambapo iliamuliwa hao wasidaiwe kwamba, kabla ya kubatizwa, watahiriwe na kukubali sheria zote 613 za Torati.

Kwa muda mfupi Kanisa lilienea Mashariki ya Kati, Ulaya Kusini, Afrika Kaskazini na kutoka huko katika ulimwengu wote uliojulikana na Wakristo wa wakati ule, hasa Dola la Roma, ingawa hilo lilijaribu kuzuia uenezi huo kwa dhuluma nyingi za kikatili kuanzia mwaka 64 hadi 313.

Baada ya uhuru wa dini kupatikana kwa hati ya Milano ni hasa wamonaki walioinjilisha Ulaya nzima hadi karne ya 14, walipoingia Ukristo watu wa Lituania[3].

Wazungu walipoanza kuvumbua maeneo ya mbali kuanzia mwisho wa karne ya 15 kwa kawaida kulikuwa na mapadri walioongozana na wapelelezi Wareno na Wahispania. Kwa wakati huo wainjilisti walianza kuitwa wamisionari, yaani watu waliotumwa kwa kazi hiyo (kutoka neno la Kilatini "missio", utume).

Uinjilishaji wa Afrika

[hariri | hariri chanzo]

Uinjilishaji wa bara hilo ulipitia hatua tatu.

Ya kwanza ilihusu Afrika Kaskazini kuanzia Misri na Sudan, lakini pia Ethiopia na nchi za jirani. Kanisa lilistawi sana na kuzaa matunda mengi: umati wa wafiadini na watakatifu wengine kama wamonaki na maaskofu bora, pamoja na teolojia na liturujia. Maendeleo hayo yalizuiwa na uenezi wa Uislamu katika karne ya 7.

Ya pili iliendana na ukoloni wa Wareno kuanzia karne ya 15 hadi karne ya 18 iliyoishia kwa kawaida kwenye vituo vyao pwani, ingawa kulikuwa na mafanikio makubwa hasa katika Ufalme wa Kongo.

Ya tatu, iliyofaulu kuenea katika bara lote, hasa Kusini kwa Sahara, ilianza mwishoni mwa karne ya 18, na kuhusisha Waprotestanti na Wakatoliki vilevile[4][5][6].

Uinjilishaji mpya

[hariri | hariri chanzo]
Siku ya kimataifa ya vijana, Copacabana (Rio de Janeiro), Brazil, 2013.

Katika Kanisa Katoliki kuanzia karne ya 20 imesisitizwa kuwa uinjilishaji unatakiwa kufanywa na waumini wote kuanzia ushuhuda wa maisha wa familia[7][8][9] [10] na kuwalenga hata waumini wenyewe, hasa wale waliojisahau katika mazingira ya uasi ya ustaarabu wa magharibi wa leo, kwa sababu Injili daima inadai wongofu, tena zaidi na zaidi[11].

  1. Timothy J. Demy Ph.D., Paul R. Shockley Ph.D., Evangelical America: An Encyclopedia of Contemporary American Religious Culture, ABC-CLIO, USA, 2017, p. 466
  2. Exhortación apostólica Evangelii Nuntiandi, Pablo VI
  3. R. Fletcher, La conversione dell'Europa. Dal paganesimo al cristianesimo, 371-1386. Milano, Tea 2003.
  4. Roswith Gerloff, Afe Adogame, Klaus Hock, Christianity in Africa and the African Diaspora: The Appropriation of a Scattered Heritage, A&C Black, UK, 2011, p. 190
  5. George Thomas Kurian, James D. Smith III, The Encyclopedia of Christian Literature, Volume 2, Scarecrow Press, USA, 2010, p. 95
  6. Martin I. Klauber, Scott M. Manetsch, Erwin W. Lutzer, The Great Commission: Evangelicals and the History of World Missions, B&H Publishing Group, USA, 2008, p. 123
  7. La Croix, Le pape François dénonce la confusion entre évangélisation et prosélytisme à l’approche du mois missionnaire extraordinaire, la-croix.com, Francia, 1 de agosto de 2019
  8. Jean-Paul Willaime et Flora Genoux, "Pour les évangéliques, l'idée reste qu'être croyant, cela doit se voir", lemonde.fr, Francia, 03 de febrero de 2012
  9. Loup Besmond de Senneville, Les protestants évangéliques revendiquent d’avoir le droit de dire leur foi, la-croix.com, Francia, 25 de enero de 2015
  10. Instrumentum Laboris, Ciudad del Vaticano, 2014
  11. Papa Fransisko, Evangelii gaudium

Tazama pia

[hariri | hariri chanzo]

Viungo vya nje

[hariri | hariri chanzo]
Makala hii kuhusu dini ya Ukristo bado ni mbegu.
Je, unajua kitu kuhusu Uinjilishaji kama historia yake, matokeo au athari zake?
Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari.