Kitubio
Kitubio au Upatanisho ni sakramenti ya Kikristo katika Kanisa Katoliki, Makanisa ya Kiorthodoksi na madhehebu mengine machache.
Kwa njia yake Mkristo aliyetubu anapokea kwa huduma ya Kanisa msamaha wa Mungu kwa dhambi alizotenda baada ya Ubatizo.
Kwa sababu hiyo, pamoja na Mpako wa wagonjwa ni kati ya sakramenti mbili za "uponyaji", zinazolenga afya ya roho na mwili inayoharibiwa na dhambi na ugonjwa.
Msingi wa teolojia yake katika Biblia
[hariri | hariri chanzo]Sakramenti za Wakatoliki na Waorthodoksi |
---|
|
Kadiri ya imani hiyo, tunaweza kuona ina msingi gani katika ufunuo, hasa Agano Jipya. Ufafanuzi wake wa kichungaji unaweza kuwa kama ifuatavyo.
Mungu aliwapa watu amri ya kusamehe dhambi kwa njia ya Mwanae. Yesu mfufuka aliwaonyesha Mitume alama ya mateso mwilini mwake, “akawavuvia, akawaambia, ‘Pokeeni Roho Mtakatifu. Wowote mtakaowaondolea dhambi, wameondolewa; na wowote mtakaowafungia dhambi, wamefungiwa” (Yoh 20:22-23). Katika Kanisa tunafurahi kupewa msamaha wa dhambi kila tunapohitaji, mradi tutubu. Kwa njia ya mwandamizi wa Mitume, Yesu anatuambia, “Umesamehewa dhambi zako... Imani yako imekuokoa, enenda zako kwa amani” (Lk 7:48,50). Si dhana wala hisia tu, bali ni neno la hakika tunalolipokea kwa masikio yetu.
Mungu aliwapa watu amri ya kusamehe dhambi zote, kwa sababu upendo mtiifu wa Mwanae aliyejitoa kuwa sadaka ya wokovu wetu unampendeza kuliko dhambi zote zinavyomchukiza. Ila hatuwezi kusamehewa dhambi ya kukataa neema ambayo Roho Mtakatifu anatusukuma tuamini na kutubu, kwa sababu pasipo imani na toba hapana msamaha. “Kila dhambi na kila neno la kufuru watasamehewa wanadamu, ila kwa kumkufuru Roho hawatasamehewa” (Math 12:31). “Nasi tukitenda kazi pamoja naye twawasihi msiipokee neema ya Mungu bure” (2Kor 6:1).
Mungu aliwapa watu amri ya kusamehe dhambi kwa sababu amependa washiriki katika kazi zake. Ametuumba kwa njia ya wazazi na kutulea na kutusaidia kwa njia ya wengine pia. Hasa ametuokoa kwa njia ya Yesu, ambaye yupo nasi sikuzote katika Mwili wake, yaani Kanisa, na katika wale walioshirikishwa mamlaka ya Mitume. “Lakini vyote pia vyatokana na Mungu, aliyetupatanisha sisi na nafsi yake kwa Kristo, naye alitupa huduma ya upatanisho; yaani, Mungu alikuwa ndani ya Kristo, akiupatanisha ulimwengu na nafsi yake, asiwahesabie makosa yao; naye ametia ndani yetu neno la upatanisho. Basi tu wajumbe kwa ajili ya Kristo, kana kwamba Mungu anasihi kwa vinywa vyetu; twawaomba ninyi kwa ajili ya Kristo: mpatanishwe na Mungu” (2Kor 5:18-20).
Hivyo, tumuendee padri ili kuondolewa dhambi tulizotenda baada ya ubatizo, kwa kuwa hatuwezi kupokea msamaha tukikataa masharti yake, na Mungu ametupangia watu ambao watuondolee kwa niaba yake. “Watu wote na watoza ushuru waliposikia hayo, waliikiri haki ya Mungu, kwa kuwa wamebatizwa kwa ubatizo wa Yohane. Lakini, Mafarisayo na wanasheria walilipinga shauri la Mungu juu yao, kwa kuwa hawakubatizwa naye” (Lk 7:29-30). Yesu mwenyewe alikubali kubatizwa na Yohane ili atimize mpango wa Baba. “Yohane alitaka kumzuia, akisema, ‘Mimi nahitaji kubatizwa na wewe, nawe waja kwangu?’ Yesu akajibu akamwambia, ‘Kubali hivi sasa; kwa kuwa ndivyo itupasavyo kuitimiza haki yote” (Math 3:14-15). Je, sisi tukatae kumkimbilia padri wa Mungu ili kupokea huruma yake tunayoihitaji kuliko hewa?
Tumuungamie padri dhambi zetu ili aweze kutushauri na kuamua kama tuko tayari kuondolewa. Tumweleze kwa unyofu makosa yote tuliyoyafanya na nia tuliyonayo ya kuyafidia na kutoyarudia. “Tukisema kwamba hatuna dhambi, twajidanganya wenyewe, wala kweli haimo mwetu. Tukiziungama dhambi zetu, Yeye ni mwaminifu na wa haki hata atuondolee dhambi zetu, na kutusafisha na udhalimu wote. Tukisema kwamba hatukutenda dhambi, twamfanya Yeye kuwa mwongo, wala neno lake halimo mwetu” (1Yoh 1:8-10). Tukumbuke tulivyo viungo vya Mwili mmoja, hivi kwamba dhambi zetu zimewadhuru wenzetu. “Ungameni dhambi zenu ninyi kwa ninyi na kuombeana, mpate kuponywa” (Yak 5:16). Kutokuwa tayari kufanya hivyo walau sirini kwa padri ni dalili ya kiburi na ya kutotubu.
Hata padri akiwa mkosefu, anaweza kutuondolea dhambi kwa niaba ya Mungu aliyempa mamlaka hiyo. Hatusamehewi na utakatifu wa padri, bali na huruma ya Baba kwa njia yake. Yeye anamtumia padri yeyote ili kuturahisishia kazi, tusihitaji kuchunguza kwanza ubora wa maisha yake, wala kwenda mbali tukampate mmoja asiye na dhambi. Tungefanyeje kuhakikisha ni mtakatifu, wakati hatuwezi kusoma moyo wake? Ingekuwa hivi, tusingepata kamwe hakika ya kusamehewa. Kumbe inatutosha kujua ni padri, kwamba Mungu amempa mamlaka ya kusamehe dhambi, kama Yesu alivyowapa Mitume siku tatu baada ya kumkimbia na hata kumkana. Kila padri anaweza kukiri, “Ni neno la kuaminiwa, tena lastahili kukubalika kabisa: ya kwamba Kristo Yesu alikuja ulimwenguni awaokoe wenye dhambi, ambao wa kwanza wao ni mimi” (1Tim 1:15). Amri ya kusamehe dhambi wamepewa watu, si malaika. “Tuna hazina hii katika vyombo vya udongo, ili adhama kuu ya uwezo iwe ya Mungu, wala si kutoka kwetu” (2Kor 4:7).
Nje ya kitubio tunaweza kuondolewa dhambi tuliyotenda baada ya ubatizo, lakini ni vigumu zaidi, kwa sababu hatupati msaada wa sakramenti hiyo maalumu. Pamoja na nia ya kumuungamia padri mapema tunahitaji neema ya kutubu kikamilifu, si kwa kuhofia adhabu, bali kwa kumpenda Mungu tuliyemchukiza. “Amesamehewa dhambi zake ambazo ni nyingi, kwa kuwa amependa sana” (Lk 7:47).
Katika maisha ya Kiroho
[hariri | hariri chanzo]Utakaso wa roho unapatikana kwa sala na kwa kufisha hisi, matakwa na maoni yetu. Lakini Mungu ametuandalia njia nyingine nyepesi na zenye nguvu za kututakasa, yaani sakramenti, ambazo zinatenda zenyewe na kusababisha neema kubwa kuliko zile tunazoweza kuzipata nje yake, mradi tuwe tayari kwa imani na upendo. Lakini kiasi cha neema zinachosababisha kinatofautiana: ni nyingi kadiri misimamo yetu ilivyo kamili; tofauti kati ya wanaopokea sakramenti ileile ni kubwa kuliko tunavyodhani. Sakramenti ya kitubio ni mojawapo kati ya njia bora za utakatifu mradi tuipokee vema, si kwa mazoea tu. Kwa ajili hiyo ni muhimu kujua namna ya kujiandaa na ya kuungama vizuri pamoja na matunda yake.
Namna ya kujiandaa
[hariri | hariri chanzo]Tunapaswa kutafiti dhamiri zetu na kuchochea majuto yetu.
Utafiti wa dhamiri unadai uangalifu mkubwa kadiri makosa ya mtu yalivyo mengi, na ujuzi wake wa hali ya ndani ulivyo mdogo. Lakini wanaojitafiti kila jioni hawakuti shida kujifahamu vema na kujihimiza wafanye bidii zote ili kujirekebisha. Watu wa Mungu ambao wanaungama mara nyingi na kujitahidi dhidi ya dhambi nyepesi za makusudi, utafiti wao wa dhamiri unahitaji muda mfupi tu. Wanapaswa kujiuliza: wiki hii kitu gani hakistahili kuandikwa na Mungu katika kitabu cha uzima? Katika nini nimekuwa wa Mungu, na katika nini nimekuwa wangu tu kwa kushindwa na hali ya nafsi, umimi, kiburi n.k.? Tukizingatia hivyo mambo kutoka juu pamoja na kuomba mwanga, tutajaliwa mara nyingi kuona maisha yetu mpaka ndani.
Hapa tutofautishe dhambi za mauti, zile nyepesi ambazo ni za makusudi kwa kiasi kikubwa au kidogo, na makosa ya udhaifu.
Ikiwa mtu anayelenga ukamilifu anatenda dhambi ya mauti katika kitambo cha udhaifu, aiungame kwa unyofu na wazi toka mwanzo wa maungamo, bila kujaribu kuificha kwa kuitaja katikati ya wingi wa dhambi nyepesi. Ni lazima aeleze idadi, aina na sababu zake, na hasa ajute kwa nia imara ya kukwepa siku za mbele si dhambi zenyewe tu, bali pia nafasi na sababu zake. Kisha kusamehewa, atunze hamu ya kufidia kwa maisha magumu na upendo. Dhambi moja ya mauti ikibaki peke yake, na kuungamwa mara na kufidiwa, inaathiri kidogo tu, hivi kwamba mtu anaweza kuendelea kupanda juu kuanzia pale alipoanguka, asilazimike kuanza na moja.
Kumbe dhambi nyepesi za makusudi ni kizuio kikubwa cha ukamilifu, hasa zikijirudiarudia kwa kuwa tumeambatana nazo. Ni maradhi halisi yanayodhoofisha roho. Bwana alimuambia Gertrude Mkuu, “Usiache dhambi izeeke ndani mwako”: dhambi nyepesi ya makusudi ni kama sumu ambayo isipotapikwa inaathiri mwili polepole, pasipo kuuua mara. Kwa mfano tusitunze kwa hiari kinyongo, wala kushikilia maoni na matakwa yetu, wala mazoea ya kusengenya au kuhukumu pasipo msingi, wala mapendo ya kibinadamu yanayoweza kuwa mtego kwetu na kutuondolea uhuru na juhudi za kumuelekea Mungu. Tukimnyima sadaka hizo anazotudai, hatuwezi kutarajia atujalie neema zinazofikisha kwenye ukamilifu. Basi tuungame wazi dhambi nyepesi za makusudi, hasa zile zinazotutia aibu zaidi. Tutafute sababu zake na kukusudia kuziepa; la sivyo ukamilifu umeacha kuwa lengo halisi kwetu. Hilo ni jambo la msingi.
Kuna dhambi nyingine tunazozitenda kwa hiari kiasi, bila kufikiria zaidi, zinazochangiwa na mishtuko na misukumo ya nafsi, ingawa utashi umeambatana nazo. Zikitokea mara nyingi ni ishara ya kwamba tunapambana kwa ulegevu, pasipo nia ya kuondoa vizuio vyote.
Kuhusu makosa ya udhaifu, utashi unahusika nayo kidogo: unayaelekea kwa muda mfupi, halafu unajirudi. Makosa hayo hatuwezi kuyaepa yote (walau mfululizo); ila tunaweza kupunguza idadi yake. Si kizuio kikubwa kwa ukamilifu, kwa kuwa yanarekebishwa mapema. Lakini inafaa kuyataja kwenye kitubio ili usafi wa roho ukamilike.
Matendo mapungufu yanatofautiana nayo kwa sababu ni upungufu tu wa juhudi za kumtumikia Mungu. Lakini, ikiwa kinadharia ni rahisi kubainisha, kiutekelezaji ni vigumu kusema upungufu wa juhudi unaishia wapi na dhambi ya uzembe inaanzia wapi. Tena, anayelenga kweli ukamilifu, hatakiwi kulegeza mwendo, si tu kukwepa asirudi nyuma. Hatimaye, matendo mapungufu yanatuelekeza kutenda dhambi nyepesi kwa kuwa hatupambani na maelekeo ya umimi kwa nguvu zinazotakiwa.
Namna ya kuungama
[hariri | hariri chanzo]Maungamo yafanywe kwa imani kubwa, tukikumbuka padri anamwakilisha Bwana. Ni hakimu (kwa kuwa sakramenti hiyo inatolewa kama hukumu: “nakuondolea”), lakini pia baba wa Kiroho na mganga anayeonyesha kwa wema dawa, mradi tumueleze vizuri maradhi yanayotusumbua. Kwa hiyo haitoshi tujishtaki kijuujuu namna isiyomfumbulia kitu, k.mf. “nimetawanya mawazo wakati wa sala”. Bali tueleze, “nimetawanya mawazo hasa kwa uzembe wakati wa ibada fulani: nimeianza vibaya, pasipo kujikusanya kwanza, au sikupambana na mawazo yaliyotokana na kinyongo au pendo la kibinadamu au masomo”. Ni vema tutaje azimio tulilowahi kuweka, halafu tuseme kama hatujalitimiza sawasawa.
Hasa tuchochee majuto yetu na kuweka azimio la kufaa ambalo litokane nayo. Kwa ajili hiyo, tufikirie sababu za kutubu. Tuombe neema ya kuelewa vema dhambi, hata nyepesi, inavyomchukiza Mungu, kwa kuwa inapinga matakwa yake; pia ni utovu wa shukrani kwa Baba aliye mwema kuliko wote: utovu ambao tunamnyima furaha ya ziada inayotupasa kumpatia na ni mbaya kadiri alivyotujalia neema. Makosa yetu yamefanya kichungu zaidi kikombe ambacho Bwana alipewa katika mateso, naye anaweza kutuambia, “Aliyetukana si adui; kama ndivyo, ningevumilia. Aliyejitukuza juu yangu siye anichukiaye; kama ndivyo, ningejificha asinione. Bali ni wewe, mtu mwenzangu, rafiki yangu, niliyejuana nawe sana. Tulipeana shauri tamu” (Zab 55:12-14). Ndizo sababu halisi za kutubu upande wa Mungu.
Upande wetu ipo nyingine: dhambi nyepesi, ingawa haipunguzi upendo, inauondolea umotomoto, uhuru wa kutenda na uenezi. Inafanya urafiki na Mungu usiwe wa ndani na tendaji zaidi. Kupoteza urafiki na mtakatifu ni hasara kubwa; lakini kupoteza urafiki wa ndani na Mwokozi hakuna kifani. Halafu dhambi nyepesi, hasa ya makusudi, inaotesha upya maelekeo mabaya na hivyo kutuandaa tutende dhambi ya mauti; na katika mambo kadhaa, mvuto wa anasa unatuvusha haraka mpaka kati ya dhambi nyepesi na ya mauti.
Kitubio kikiadhimishwa hivyo, kwa nguvu ya maondoleo na kwa mashauri ya padri, kitakuwa chombo kikubwa kwa utakatifu. [1]
Matunda ya kitubio
[hariri | hariri chanzo]Ni matunda ya maadili ya unyenyekevu na toba, na hasa ya maondoleo. Tendo lipi la unyenyekevu ni halisi na la lazima kuliko lile la kukiri kwa unyofu makosa tuliyotenda? Ndiyo dawa ya kiburi, kilicho asili ya dhambi zote. Ndiyo sababu uzushi, ambao ni tunda la kiburi, umefuta kitubio. Dhambi za kiburi zinaanza kufidiwa tayari na maungamo manyenyekevu. Tendo la toba linalaumu na kukataa dhambi iliyotendwa kwa kuwa imemchukiza Mungu: hivyo mtu anamrudia Bwana wake, ambaye alimuacha kwa dhambi ya mauti, au walau alisogea mbali naye kwa dhambi nyepesi. Anamkaribia tena na kujitupa kwa upendo na tumaini mikononi mwa huruma yake. Hasa kwa maondoleo damu ya Mwokozi inamwagwa kisakramenti juu ya roho yetu. Mwingine asiye na kitubio, kama ametenda dhambi zisizomuacha atulie, hapati kamwe faraja ya kumsikia mtumishi wa Mungu akimuambia kwa niaba yake, “Nakuondolea dhambi zako”. Hapati faraja ya kuona anavyohusika na neno la Mwokozi kwa mitume wake, “Wowote mtakaowaondolea dhambi, wameondolewa” (Yoh 20:23). Kumbe katika sakramenti damu azizi ni dawa bora ambayo, ikiunganisha nguvu yake na unyenyekevu na toba, inaondolea dhambi, na kuchangia uponyaji kamili wa roho. “Kwa njia ya kitubio hampati tu maondoleo ya dhambi nyepesi, bali pia nguvu kubwa ya kuziepa siku za mbele, mwanga mkali kwa kuzitambua, na wingi wa neema kwa kufidia hasara zote zilizosababishwa nazo” (Fransisko wa Sales).
Lakini matokeo ya maondoleo yanalingana daima na ubora wa misimamo tunayopokea sakramenti, kwa kuwa kati ya watu wanaoungama Mungu anang’amua tofauti ambazo hakuna anayeweza kuzihisi. Kuna viwango vingi vya unyenyekevu, majuto na upendo wa Mungu, kama viwango vya joto la mwali. Hiyo ni kweli pia kuhusu malipizi ya sakramenti, ambayo yana thamani kuliko mengine kwa kuwa matokeo yake yanategemea sakramenti, lakini kipimo chake kinategemea juhudi katika kuyafanya, hivyo yanatuondolea kwa kiasi tofauti adhabu tuliyostahili kwa dhambi tulizoondolewa. Kwa hiyo tusiahirishe malipizi, bali tuwahi kuyafanya na kumshukuru Mungu kwa maondoleo. Damu ya Yesu imetiririka rohoni mwetu ili kuitakasa; tumuombe tudumu mpaka kufa katika hali ya neema. Watakatifu tu wanajua thamani ya damu hiyo. Jinsi ilivyo kubwa neema ya kuangaziwa vilindi vya fumbo la ukombozi!
Hatimaye inafaa tujishtaki walau kwa jumla kuhusu dhambi za zamani, kwa kuzifikiria zile kubwa zaidi, ili tuzidi kuzijuta na kusudi stahili za Yesu, zikihusishwa na dhambi hizo zilizokwishaondolewa, zipunguze adhabu ya muda ambayo kwa kawaida inatupasa bado. “Ni nani awezaye kuyatambua makosa yake? Unitakase na mambo ya siri” (Zab 19:12), yanayotegemea hiari kiasi, kutokana na uzembe wangu katika kujua na kutaka yale yanayonipasa niyajue na kuyataka.
Bwana alimuambia Veronika Giuliani, “Utasonga mbele katika ukamilifu kadiri utakavyochuma matunda ya sakramenti hii”. Fransisko wa Sales anatushauri, “Muwe makini sana… kusikiliza rohoni mwenu maneno ya maondoleo ambayo Mwokozi wa roho zenu anatamka kutoka juu mbinguni wakati uleule ambao mtumishi wake anawaondolea hapa duniani kwa niaba yake… Hakuna tabia ngumu kiasi kwamba isiweze kutawaliwa na kurekebishwa, kwanza kwa neema ya Mungu, halafu kwa juhudi na bidii. Katika hayo mfuate maagizo na mwenendo wa kiongozi aliyejaa ari na busara”. Mtakatifu huyo aling’amua kuwa majuto halisi hayakatishi tamaa kamwe, bali ni huzuni takatifu ambayo inaandaa roho kufanya bidii, na inainua moyo kwa sala na tumaini, hata uruke kwa ari: “katika ukubwa wa uchungu wake inazaa daima utamu wa faraja isiyo na kifani”. Ikiwa huzuni ya majuto ina utamu huo, ni kwa sababu inatokana na upendo. Kadiri tunavyoona uchungu kwa makosa yetu, tuna hakika ya kumpenda Mungu. Katika huzuni hiyo yanapatikana matunda ya Roho Mtakatifu: “upendo, furaha, amani, uvumilivu, utu wema, fadhili, uaminifu, upole, kiasi” (Gal 5:22-23).
Tanbihi
[hariri | hariri chanzo]- ↑ Anjela wa Foligno alipotambua dhambi zake alishikwa na hofu kubwa ya kulaaniwa milele, akalia machozi kwa uchungu, lakini hakuziungama. “Mara nyingi alipokea ekaristi katika hali ya dhambi kwa sababu aliona aibu kubwa mno kuungama kikamilifu. Usiku na mchana dhamiri yake ilimsuta. Alimuomba Mt. Fransisko amtafutie muungamishi aliyejua vizuri dhambi, ili aweze kumuungamia kikamilifu... ‘Nikaungama inavyotakiwa’... bila kuona upendo, ila uchungu... akafanya malipizi ili kumpa Mungu fidia ya dhambi zake, huku akijikuta bado amejaa uchungu... Akazidi kuzingatia huruma ya Mungu iliyomjalia huo msamaha na kumtoa motoni mwa milele. Akaanza kupata mwanga; hapo uchungu na machozi vikazidi kuliko awali, akajiachia kufanya malipizi makali zaidi na zaidi... Kwa mwanga huo wa kiasi akaona ndani mwake dhambi tu, akajihukumu mbele ya Mungu kuwa kwa hakika amestahili moto wa milele... ‘Faraja yangu pekee ilikuwa kuweza kulia machozi... Mwanga fulani ukanijalia kutambua kwa dhati zaidi dhambi zangu zote. Kwa mwanga huo niliona kwamba nilivichukiza viumbe vyote vilivyoumbwa kwa ajili yangu... Niliomba watakatifu wote na bikira Maria waniombee na kusihi ule Upendo ambao uliwahi kunijalia fadhili kubwa hivyo uhuishe kilichokuwa kimekufa ndani mwangu. Kama matokeo nilijisikia kufikiwa na huruma ya viumbe vyote na watakatifu wote... Nikajaliwa ujuzi mkubwa zaidi wa jinsi Mwana wa Mungu alivyokufa kwa dhambi zetu. Ujuzi huo ulinifanya ning’amue kwa uchungu mkubwa sana dhambi zangu zote. Nikatambua kuwa aliyemsulubisha Kristo ni mimi mwenyewe... Halafu Bwana, kwa huruma yake, akanitokea mara nyingi, katika usingizi na katika kukesha, akiwa daima msalabani. Akaniambia nitazame madonda yake... Alikuwa akihesabu moja moja mapigo ya mijeledi aliyopata, akaniambia, ‘Nimevumilia hayo yote kwa ajili yako’... Nikawasihi bikira Maria na mtume Yohane waniombee nipate neema ya kuonya daima chochote cha uchungu wa mateso ya Kristo, au walau cha yale waliyojaliwa wao. Wakanipatia na bado wananipatia fadhili hiyo, hata siku fulani Mt. Yohane akanishirikisha kiasi kwamba uchungu huo ulipita mwingine wowote niliowahi kupata’”. Kwa majuto hayo Anjela alishika njia ya utakatifu. Neema kubwa alizojaliwa zituvute kuzingatia misaada ambayo Bwana anatutolea kila siku, na makuu yaliyomo katika maisha ya Kikristo ya kawaida.
Makala hii kuhusu dini ya Ukristo bado ni mbegu. Je, unajua kitu kuhusu Kitubio kama historia yake, matokeo au athari zake? Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa? Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari. |