[go: up one dir, main page]

Nenda kwa yaliyomo

Kipaimara

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
Askofu akitoa Kipaimara. Mchoro wa Rogier van der Weyden, Sakramenti saba, karne ya 15.


Kipaimara ni ibada ya madhehebu mbalimbali ya Ukristo inayolenga kumthibitisha mwamini katika kumfuata Yesu kwa uweza wa Roho Mtakatifu.

Katika mpangilio wa sakramenti saba

[hariri | hariri chanzo]
Sakramenti za Wakatoliki na Waorthodoksi

Kadiri ya Kanisa Katoliki na Waorthodoksi ubatizo hautoshi, bali unahitaji kukamilishwa na kipaimara na ekaristi, kama vile baada ya kuzaliwa tunahitaji kukomaa na kudumisha uhai wetu kwa chakula. Sakramenti hizo tatu kwa pamoja ni msingi wa maisha ya Wakristo wote, kumbe nyingine zinahitajika tu katika hali na nafasi maalumu.

Mitume wa Yesu waliwaendea Wasamaria “wakawaombea wampokee Roho Mtakatifu; kwa maana bado hajawashukia hata mmoja wao, ila wamebatizwa tu kwa jina lake Bwana Yesu. Ndipo wakaweka mikono yao juu yao, nao wakampokea Roho Mtakatifu” (Mdo 8:15-16). “Amin, amin, nawaambieni: Msipoula mwili wake Mwana wa Adamu na kuinywa damu yake, hamna uzima ndani yenu” (Yoh 6:53).

Sakramenti inayohusiana zaidi na ubatizo ni kipaimara, kinachoendeleza kazi yake. “Waliposikia haya wakabatizwa kwa jina la Bwana Yesu. Na Paulo, alipokwisha kuweka mikono yake juu yao, Roho Mtakatifu akaja juu yao” (Mdo 19:5-6). Sakramenti hizo ni kama pande mbili za pesa moja. Zinahusiana kama Pasaka na Pentekoste, ambayo ni utimilifu wake, kwa kuwa siku alipofufuka Yesu aliwapulizia Mitume Roho Mtakatifu, ambaye siku hamsini baadaye akawajia kama “upepo wa nguvu ukienda kasi, ukaijaza nyumba yote” (Mdo 2:2).

Kwa Kanisa Katoliki, Waorthodoksi na wengineo Kipaimara ni sakramenti ya pili katika safari ya kuingizwa katika Ukristo ambayo inaanza kwa Ubatizo na kukamilishwa na Ekaristi. Kwa kawaida sakramenti hizo tatu zilikuwa zikitolewa pamoja, lakini baadaye Kanisa la Magharibi lilizidi kuzitenganisha, hasa kwa lengo la kumuachia askofu tu adhimisho la kipaimara.

Kwa kuwa hii ni hasa ibada ya Roho Mtakatifu, ishara yake ni tendo la kuwekea mkono kichwani, inayomaanisha kumuita juu ya mhusika.

Pamoja na kuwekea mikono na mwandamizi wa Mitume, kwa Wakatoliki na Waorthodoksi ni lazima pia kupaka paji la uso kwa mafuta ya kunukia (yanayoitwa "krisma") pamoja na kutamka maneno yanayoweka wazi kwamba ndiye anayetolewa kama paji na mhuri wa kuwa mali ya Bwana. Ndiyo inayowafanya watu waitwe Wakristo nyuma ya Yesu aliyeitwa Kristo. “Kwa sababu huyo ndiye aliyetiwa muhuri na Baba, yaani, Mungu” (Yoh 6:27). “Yeye atufanyaye imara pamoja nanyi katika Kristo, na kututia mafuta, ni Mungu, naye ndiye aliyetutia muhuri akatupa arabuni ya Roho mioyoni mwetu” (2Kor 1:21-22).

Madondoo mengine yanayozungumzia mpako na mafuta kuhusiana na Ubatizo ni 2Kor 1:21 na 1Yoh 2:20,27.

Neema ya kipaimara

[hariri | hariri chanzo]

Kumpokea Roho Mtakatifu maana yake ni kuja kuongozwa naye badala ya kutawaliwa na shetani. “Kwa kuwa ninyi mmekuwa wana, Mungu alimtuma Roho wa Mwanae mioyoni mwetu, aliaye, ‘Aba!’ yaani, ‘Baba!’ Kama ni hivyo, wewe si mtumwa tena bali u mwana; na kama u mwana, basi, u mrithi kwa Mungu. Lakini wakati ule, kwa kuwa hamkumjua Mungu, mliwatumikia wao ambao kwa asili si miungu... Tukiishi kwa Roho, na tuenende kwa Roho” (Gal 4:6-8; 5:25). “Ikiwa Roho wa Mungu anakaa ndani yenu, ninyi hamwufuati mwili; bali mwaifuata roho. Lakini mtu awaye yote asipokuwa na Roho wa Kristo, huyo si wake” (Rom 8:9).

Tukimpokea Roho Mtakatifu papo hapo tunapokea pia adili kuu la upendo: “Pendo la Mungu limekwisha kumiminwa katika mioyo yetu na Roho Mtakatifu tuliyepewa sisi” (Rom 5:5). Tena tunapokea vipaji vyake ambavyo Yesu alikuwa navyo kikamilifu. “Roho ya Bwana atakaa juu yake, roho ya hekima na ufahamu, roho ya shauri na uweza, roho ya maarifa na ya kumcha Bwana. Na furaha yake itakuwa katika kumcha Bwana” (Isa 11:2-3). Mambo hayo, tofauti na karama, ni ya lazima kwa yeyote apate wokovu wa milele.

Tunda la kuongozwa na Roho Mtakatifu ni umoja wa Kanisa unaotokana na ustawi wa upendo na vipaji ndani ya waamini. “Wote walijaa Roho Mtakatifu, wakanena neno la Mungu kwa ujasiri. Na jamii ya watu walioamini walikuwa na moyo mmoja na roho moja” (Mdo 4:31-32). “Tunda la Roho ni upendo, furaha, amani, uvumilivu, utu wema, fadhili, uaminifu, upole, kiasi; juu ya mambo kama hayo hakuna sheria” (Gal 5:22-23). “Lakini, mkiwa na wivu wenye uchungu na ugomvi mioyoni mwenu, msijisifu, wala msiseme uongo juu ya kweli. Hekima hiyo siyo ile ishukayo kutoka juu, bali ni ya dunia, ya tabia ya kibinadamu, na Shetani. Maana hapo palipo wivu na ugomvi, ndipo palipo machafuko, na kila tendo baya. Lakini hekima itokayo juu, kwanza ni safi; tena ni ya amani, ya upole, tayari kusikiliza maneno ya watu, imejaa rehema na matunda mema, haina fitina, haina unafiki” (Yak 3:14-17).

Makala hii kuhusu dini ya Ukristo bado ni mbegu.
Je, unajua kitu kuhusu Kipaimara kama historia yake, matokeo au athari zake?
Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari.