[go: up one dir, main page]

Mungu ni jina lenye asili ya Kibantu linalotumika kwa yeyote anayesadikiwa katika dini mbalimbali kuwa na uhai wa hali ya juu.

Alama ya Wasumeri iliyomaanisha dingir, mungu (mmojawapo).
Mabadiliko ya uandishi wa herufi nne za Kiebrania YHWH, jina maalumu la Mungu katika Biblia ya Kiebrania.
Jina la Allah, Mungu, kwa herufi za Kiarabu.

Kati ya wafuasi wa dini hizo, wengi wanaona kuwa Umungu, kwa jinsi ulivyo au unavyofirika, haukubali mgawanyiko. Hasa katika Uyahudi, Ukristo na Uislamu wanasisitiza umoja wa Mungu kuwa ndio msingi wa imani yao. Kwao Mungu ni wa milele, anafahamu yote na kutaka hasa uwepo wa viumbe. Tena kwa hiari yake alipenda kujifunua kwa binadamu; kielelezo ni Ibrahimu/Abrahamu aliyefanywa rafiki yake na baba wa waamini wote.

Kuna dini nyingine zinazokubali kuwepo kwa miungu mbalimbali (wawili au zaidi). Hasa dini nyingi za jadi zinaamini wingi wa miungu. Dini kubwa duniani inayosadiki miungu mingi ni Uhindu. Pia katika sehemu za Afrika ya Magharibi ibada za miungu mingi zinaendelea hadi leo.

Mungu na miungu katika dini asilia za Kiafrika

Jamii za Afrika zilikuwa na dini zao ambamo tunaweza kuona imani katika nguvu za kiroho ambazo zinaitwa majina tofauti. Tunaweza kukuta imani ya Mungu Mkuu, pia ya miungu mbalimbali, pamoja na imani ya kuwepo kwa roho za wahenga, mizimu na pepo mbalimbali.

Tukijiuliza juu ya uhusiano kati ya mizimu, roho, miungu mbalimbali na Mungu Mkuu, ni lazima kwanza tujue imani za jadi hutofautiana kutoka jamii moja hadi jamii nyingine.

Mara ningi imani za Kiafrika humwona Mungu Mkuu mmoja kuwa wa juu na mwenye nguvu zaidi. Yuko kabla ya kila kitu kingine na asili yake haijulikani. Hivyo nguvu hutazamwa kwa ngazi tofauti; Mwenyezi Mungu yuko juu, chini yake kuna roho mbalimbali au hata miungu pamoja na nguvu za asili, na mwishoni binadamu wasio na nguvu nyingi.

Wakati mwingine hadithi za uumbaji za Kiafrika zinamwonyesha Mungu akiwa au akienda mbali na watu au hawasiliani nao tena moja kwa moja. Anaacha washughulikiwe na roho au miungu midogo aliyoumba pia. Mungu wa aina hiyo anaonekana mbali sana na mambo ya binadamu; kwa sababu hiyo, mara kwa mara miungu midogo huombwa badala yake ili kupata usaidizi. Katika jamii nyingine wanaamini kwamba mizimu inaweza kuleta mawasiliano baina ya Mungu na binadamu.

Vikundi vingine humwona Mungu Mkuu kuwa karibu sawa na miungu mingine, kama mwenyekiti wao au kama mfalme kati ya machifu. Wafon katika Afrika ya Magharibi humwaza Mungu mkuu kama mapacha mawili: Mavu, nguvu ya kike, na Lisa, nguvu ya kiume. Wakitazamwa kama nguvu moja huitwa Mavu pekee. Wameumba watoto ambao hutawala shughuli za dunia na viumbe vyake kama miungu.

Dhana za aina hiyo zimeleta majadiliano kati ya wataalamu kuhusu kuainisha dini za Kiafrika kuwa za Mungu mmoja (monotheistic) au za miungu mingi (polytheistic). Wengine huona uainishaji huo hauna maana kwa dini za Kiafrika.

Mtaalamu John Mbiti wa Kenya aliona kwamba kimsingi imani katika Mungu mmoja inapatikana kwa namna moja au nyingine katika dini zote za asili. Anaeleza nguvu nyingine za kiroho kama tabia au shughuli za Mungu yeye yule zinazotazamwa pekepeke.

Mungu katika Biblia

Biblia inaanza kwa kukiri kwamba asili ya uhai wote ni Mwenyezi Mungu: “Hapo mwanzo Mungu aliziumba mbingu na nchi” (Mwa 1:1).

 
Mesha Stele ni jiwe la zamani lililoandikwa mwaka 840 KK na ni ushahidi wa kwanza kufahamika wa Mungu wa Israeli, Yahweh.

Tena, kwamba Mungu anazidi kushughulikia viumbe vyake, akividumisha na kuviongoza vyote vifikie lengo alilovipangia. “Ndani yake yeye tunaishi, tunakwenda na kuwa na uhai wetu” (Mdo 17:28). Tunamtegemea pande zote: angetuacha kidogo tungetoweka mara. Yesu alipolaumiwa kwa kuponya watu siku ya pumziko, alijitetea kwamba, “Baba yangu anatenda kazi hata sasa, nami ninatenda kazi” (Yoh 5:17). "Yeye hujishughulisha sana kwa mambo yenu" (1Pet 5:7).

Kutokana na imani hiyo, tunahimizwa kujiachilia mikononi mwake kwa moyo wa kitoto, tukiwajibika bila mahangaiko yanayowapata watu wasiomjua. “Waangalieni ndege wa angani, ya kwamba hawapandi, wala hawavuni, wala hawakusanyi ghalani; na Baba yenu wa mbinguni huwalisha hao. Ninyi je, si bora kupita hao?” (Math 6:26). “Nawe una nini usichokipokea?” (1Kor 4:7). “Nimrudishie Bwana nini kwa ukarimu wake wote alionitendea?” (Zab 116:12).

Tunaanza kumjua Mungu kwa kuzingatia viumbe vyake, hasa dhamiri yetu. “Kwa sababu mambo yake yasiyoonekana tangu kuumbwa ulimwengu yanaonekana, na kufahamika kwa kazi zake; yaani, uweza wake wa milele na Uungu wake” (Rom 1:20).

Hivyo tunaweza pia kusema juu ya Mungu kuanzia wema, ukweli na uzuri wa viumbe vyake na kumsifu kiasi chetu kwamba ndiye wema, ukweli na uzuri wenyewe. Lakini tukiri pia kuwa maneno yetu duni hayawezi kutosha kamwe kufafanua fumbo lake. “Kwa maana, nimesema maneno nisiyoyafahamu, mambo ya ajabu ya kunishinda mimi, nisiyoyajua” (Ayu 42:3). Tungemuelewa, asingekuwa Mungu.

Mwenyezi Mungu ni ukamilifu mtupu usio na mipaka kwa milele yote. “Tazama, Mungu ni mkuu, nasi hatumjui; hesabu ya miaka yake haitafutiki” (Ayu 36:26). “Mungu ni Roho, nao wamwabuduo yeye imewapasa kumwabudu katika roho na kweli” (Yoh 4:24).

Akiwa Roho, viungo ambavyo pengine anapewa vinamaanisha tu sifa fulani: k.mf. macho ujuzi wake, mikono uwezo wake, mabawa ulinzi wake, n.k. “Roho haina mwili na mifupa” (Lk 24:39).

Hasa Mungu amejifunua kuwa upendo wenyewe. “Bwana, Bwana, Mungu mwingi wa huruma, mwenye fadhili, si mwepesi wa hasira, mwingi wa rehema na kweli” (Kut 34:6). “Mungu ni upendo, naye akaaye katika pendo, hukaa ndani ya Mungu, na Mungu hukaa ndani yake” (1Yoh 4:16). “Yeye asiyependa, hakumjua Mungu, kwa maana Mungu ni upendo” (1Yoh 4:8).

Marejeo

  • Pickover, Cliff, The Paradox of God and the Science of Omniscience, Palgrave/St Martin's Press, 2001. ISBN 1-4039-6457-2
  • Collins, Francis, The Language of God: A Scientist Presents Evidence for Belief, Free Press, 2006. ISBN 0-7432-8639-1
  • Miles, Jack, God: A Biography, Vintage, 1996. ISBN 0-679-74368-5
  • Armstrong, Karen, A History of God: The 4,000-Year Quest of Judaism, Christianity and Islam, Ballantine Books, 1994. ISBN 0-434-02456-2
  • Paul Tillich, Systematic Theology, Vol. 1 (Chicago: University of Chicago Press, 1951). ISBN 0-226-80337-6
  • Hastings, James Rodney (2nd edition 1925–1940, reprint 1955, 2003) [1908–26]. Encyclopedia of Religion and Ethics. John A Selbie (tol. la Volume 4 of 24 ( Behistun (continued) to Bunyan.)). Edinburgh: Kessinger Publishing, LLC. uk. 476. ISBN 0-7661-3673-6. The encyclopedia will contain articles on all the religions of the world and on all the great systems of ethics. It will aim at containing articles on every religious belief or custom, and on every ethical movement, every philosophical idea, every moral practice. {{cite book}}: |access-date= requires |url= (help); Check date values in: |year= (help)

Viungo vya nje

WikiMedia Commons 
WikiMedia Commons
Wikimedia Commons ina media kuhusu:
  Makala hii kuhusu mambo ya dini bado ni mbegu.
Je, unajua kitu kuhusu mada hii kama historia yake au uenezi wake?
Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari.