[go: up one dir, main page]

Nenda kwa yaliyomo

Ndovu

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
Ndovu
Ndovu au Tembo
Ndovu au Tembo
Uainishaji wa kisayansi
Himaya: Animalia (Wanyama)
Faila: Chordata (Wanyama wenye ugwe wa neva mgongoni)
Ngeli: Mammalia (Wanyama wenye viwele wanaonyonyesha wadogo wao)
Oda: Proboscidea (Wanyama wenye mwiro)
Familia: Elephantidae (Wanyama walio na mnasaba na ndovu)
Ngazi za chini

Jenasi 2

Msambao wa Ndovu wa Afrika (kijani) na Ndovu wa Asia (kahawia).
Msambao wa Ndovu wa Afrika (kijani) na Ndovu wa Asia (kahawia).

Ndovu au tembo ni aina za wanyama wenye umbo kubwa kupita wanyamapori wote wa ardhi. Watoto wake wakizaliwa hufikia kg 100 na ndovu mzima huwa na uzito wa tani 2 hadi 5; kimo ni hadi m 4.

Kibiolojia ni mamalia. Sehemu ya pekee mwilini ni mwiro ambao hali halisi ni pua la tembo lililorefuka na kufanya kazi pia kama mkono, yaani kwa kutumia mwiro ndovu hushika vitu na kufanya utafiti kwa kugusagusa.

Pembe-jino zake zinatafutwa sana kama mapambo na biashara ya pembe za ndovu imeshakuwa hatari kabisa kwa ndovu wote kwa sababu wanawindwa mno. Hivyo kwa mapatano ya kimataifa biashara ya pembe hizi imepigwa marufuku.

Utangulizi

[hariri | hariri chanzo]

Tembo ni mamalia wakubwa wa jenasi Elephas na ‘Loxodonta’ za familia ya ‘Elephantidae’. Kuna spishi tatu tu za tembo zinazoishi mapaka leo: Ndovu-nyika au tembo wa vichakani wa Afrika (African Bush Elephant), ambao ni mkubwa kuliko wengine; tembo wa misituni wa Afrika (African Forest Elephant) na tembo wa Asia (Asian Elephant). Wanafanana lakini hawazaliani. Ndovu-misitu alitazamwa muda mrefu kama nususpishi ya Ndovu wa Afrika lakini wataalamu wamethibitisha ni spishi tofauti. Hufikia kimo cha mita 2 tu; anaishi hasa katika misitu ya Kongo. Spishi nyingine zote za tembo zimekoma.

Tembo ndiyo mamalia wa nchi kavu wakubwa kuliko wote sasa. Tembo hubeba mimba kwa miezi 22, muda mrefu kuliko wanyama wote wa ardhini. Ndama wa tembo akizaliwa huwa na uzito wa kilogramu 120. Tembo huishi kwa miaka 50-70, lakini tembo aliyevunja rekodi aliishi miaka 82.

Tembo mkubwa kupata kuishi alikuwa huko Angola na kupigwa risasi mnamo mwaka 1956. Tembo dume huyu alikuwa na uzito wa kg. 12,000, akiwa na kimo mpaka mabegani cha mita 4.2, mita moja zaidi kuliko tembo wa sasa wa Africa. Tembo wadogo, kama saizi ya ndama, au nguruwe mkubwa, waliishi zamani sana, huko visiwa vya Crete.

Tembo wametokea sana kwenye tamaduni za dunia. Ni ishara/alama ya hekima huko Asia na ni maarufu kwa uwezo wao wa kumbukumbu na akili, ambapo hufanikiwa kukaribiana na jamii ya binadamu wa kale. Mwanafalsafa Aristotle aliwahi kusema ndiye “mnyama pori anayewapiku wengine wote kwa hekima na akili”. Jina la tembo kwa Kiingereza lina asili ya neno la Kigiriki lenye maana ya meno/pembe za ndovu.

Tembo wakubwa hawana wanyama wanaowawinda ingawa simba huweza kuwashambulia ndama wa tembo na tembo wadhaifu. Japokuwa hutishiwa sana na kuwa hatarini kutokana na mwingiliano na binadamu na ujangili. Kadiri ya sensa ya mwaka 2007, tembo wa Afrika walikuwa kati ya 470,000 au 690,000. Tembo hulindwa duniani kote. Hii ni sambamba na maeneo maalumu ya kuwakamata, matumizi ya nyumbani na biashara kwenye mazao yake kama viel vipusa. Mataifa kadhaa yameripoti kupungua kwa tembo wao mpaka kufikia theluthi mbili, na hata wale walio kwenye maeneo tegefu nao wako hatarini kutoweka kutokana na kuongezeka kwa ujangili kwa zaidi ya asilimia 45% kupelekea hata takwimu za sasa kutokuwepo.

Viunzi vya tembo na mtu.

Tembo wana ngozi pana sana kwenye asilimia kubwa ya msuli wao na hukaribia sentimeta 2.5 kwa upana. Japo ngozi kwenye mdogo na sikioni ina upana wa karatasi tu. Ngozi ya tembo wa Asia huwa na nywele kiasi, hasa wakati wa utoto na kupungua wakati wanapoendelea kukua; huku tembo wa Afrika wakiwa hawana nywele kabisa.

Tembo

Tembo hutuma mkonga kwa kazi mbali mbali mojawapo kupukuta jicho lake. Mkonga ni muunganiko wa pua na mdomo wa juu, umenyooka na kuwa ogani muhimu kwa tembo. Tembo wa Afrika wana vitu kama vidole viwili hivi mwishoni mwa mikongo yao, huku tembo wa Asia wakiwa na kimoja tu. Kulingana na wanabiolojia, mkonga wa tembo unatakribani ya misuli 40,000 ndani yake, inayoifanya uwe na uwezo wa hata kuinua kipande kidogo cha kioo, vile vile kuwa na nguvu za hata kung’oa matawi ya misuli ndani ya mkonga wa tembo ni karibu ya 100,000 wanyama wengi wala majani hutumia meno yao chonge kurarua na kuchana majani. Hata hivyo, isipokuwa kwa wakiwa bado wadogo, tembo hutumia mikonga yao kuchuma chakula na kuweka kinywani mwao. Hula majani, matunda na matawi yake huangusha mti wote kabisa. Mkonga wa tembo hutumika pia kunywea maji. Tembo huvuta maji kupitia tundu za mkonga wake, mapaka lita kumi na nne kwa wakati mmoja, na kuyamimina kinywani mwake. Wakati mwingine hujimwagia maji mwilini kwa maana ya kuoga. Pia huweza kujipaka vumbi na tope, ambapo pindi hukauka huwa kama namna ya kujikinga na mwanga mkali wa jua. Wakati wa kuogelea, mkonga huwa kama neli yam zamia huwa nzuri kweli kweli. Mkonga pia hufanya kazi kubwa katika mahusiano ya jamii yake na wanyama wengine. Tembo husalimiana kwa kukutanisha na kuishikisha mkonga yao, sawia na binadamu anayosaliamana kwa kushikana mikono. Huitumia mikonga yao wakti wa kupishana, kupapasana na wenzi na pia mama anapoluwa anambembeleza mtoto. Pia pindi anapoinua mkonga wake humaanisha kusalimu amri. Tembo hujilinda wenyewe kutoka kwa wavamizi kwa kuwadaka na kuwabana.

Tembo pia hutegemea mkonga kwa ajili ya kunusa. Kwa kuinua mkonga hewani na kuyumbisha pande zote, na kama peviskopu, mkonga hutumika kutambua marafiki, maaduai na vyanzo vya chakula.

Pembe (au pembe-jino)

[hariri | hariri chanzo]

Pembe za tembo ni kama meno ya pili ya chonge ya tembo hawa. Pembe hukua mfululizo, na kwa mwaka mmoja, huongezeka kwa sm 18 kwa tembo dume. Pembe hizi hutumika kuchimba kwa ajili ya maji, chumvi, mizizi, kula magome ya miti, na kutaboa miti ya mibuyu kupata majimaji ya ndani. Pia hutumika kusafisha njia kwa kusogeza na kukata miti na matawi ya miti mikubwa. Pia hutumika kuweka alama kwenye miti kuonyesha mipaka ya hiamaya zao na mara kadhaa hutumika kama silaha.

Kama ilivyo kwa binadamu, wanapokuwa wanazoea kutumia sana mkono wa kulia ama kwa wengine wa kushoto, vivyo hivyo tembo nao huwa na ubobezi katika kutumia aidha pembe ya kushoto au kulia. Pembe inayotumika sana, huitwa penge kuu, kuwa fupi kidogo, na iliyolika kidogo kwenye ncha yake kutokana na matumizi. Tembo wote wa Afrika, dume na jike, huwa na pembe kubwa zinazoweza kufikia mita 3 kwa urefu na uzito wa kilo tisini. Tembo wa Asia huwa na pembe kwa dume pekee, lakini pembe zao huwa nyembamba na nyepesi, huku nzito kuliko zote kwao ilikuwa na uzito wa kg 39 Pembe kwa spishi zote huundwa kwa kalsiamu fosfeti, huku sehemu ya tishu hai ikiwa ni ndogo mno. Watu hutaka kupata pembe za tembo kwa wingi nao kumepelekea sana kuadimika kwa tembo hao kutokana na uwindaji wa tembo.

Kwa sababu ya ujangili wa ndovu ili kupata pembe zao aina za ndovu bila pembe zimetokea kwa mahali mbalibali, kaskazini kwa Msumbiji hasa. Ndovu hawa huitwa buda.

Meno ya tembo ni tofauti sana na yale ya mamalia wengine. Wakati wa maisha yao yote, huwa na jumla ya meno 28. Haya hujumuisha meno change ba pili (hizi ndizo pembe), meno ya maziwa kabla ya pembe, magego madogo 12:3 kila upande wa taya, magego 12:3 kila upande wa taya.

Tembo hifadhi ya Taifa Saadani

Upande wa taya

[hariri | hariri chanzo]

Tofauti na mamalia wengine ambao meno ya kitoto huanza na kupisha meno ya ukubwani ya moja kwa moja, tembo huwa na mzunguko wa meno kwa maisha yao yote. Pembe zao hutanguliwa na meno change mawili ambayo huondoka baada ya mwaka mmoja na pembe kuchomoza. Magego hubadilishwa walau mara tano katika maisha ya tembo. Meno hayatoki kutaka kwenye fidhi wima kama kwa binadamu isipokuwa, kutoka kwa ulalo, kama mkanda wa kusukumia mashine. Meno mapya hukua nyuma ya kinywa na kuyasukuma meno ya zamani nje. Tembo wanapozeeka sana, ile seti ya mwisho ya meno huisha na kuwa laini hata kushindwa tena kula na kutafuana na kutegemea tu chakula laini tu. Tembo hao wazee hutumia muda wao wa siku za mwisho kwenye maeneo wazi ambako wanaweza kula nyasi laini. Kwa bahati mbaya, meno yao ya mwisho yanapodondoka, tembo hao hushindwa kula na hufa kwa njaa. Isingekuwa kuisha kwa meno, tembo wangekuwa na uwezo wa kuishi kwa muda mrefu sana. Kwa sababu sasa makazi ya tembo yanazidi kuvamiwa na kuwa madogo mno, tembo wazee hukosa sehemu nzuri za kujipatia nyasi laini na hivyo hufa mapema kwa njaa.

Ndovu hula manyasi na majani mengi. Kwa chakula hiki ambacho ni kigumu hutegemea meno yao. Meno hayo polepole yanachakaa kutokana na ugumu wa manyasi na baada ya kuharibu meno yote ndovu hufa.

Penye ndovu wengi mno wanaharibu miti. Wanapenda majani ya miti na hivyo wanavunja matawi ili wapate majani. Wakiweza wanaangusha pia mti wote kwa chakula hiki. Uharibifu huu ni tatizo katika mbuga za wanyama kadhaa ambako ndovu hawawezi kutoka nje kwa sababu nje wanawindwa.

Spishi za Afrika

[hariri | hariri chanzo]

Spishi ya Asia

[hariri | hariri chanzo]

Tembo wa Afrika

[hariri | hariri chanzo]
Ndovu-nyika - Mikumi.

Tembo wa jenasi ya ‘Loxodonta’, kwa ujumla hujulikana kama tembo wa Afrika. Kwa sasa wanapatikana katika nchi 37. Tembo wa Afrika hutofautishwa na tembo wa Asia kwa namna mbali mbali. Kwanza masikio yao ni makubwa sana na mwili wao ni mkubwa wenye mgongo uliopinda. Wote, dume na jike wa tembo wa Afrika huwa na pembe za ndovu/vipusa kwa nje na miili yao huwa na nywele kidogo kuliko tembo wa Asia.

Ndovu wa Afrika hugawanywa kwenye makundi mawili kulingana na spishi zao, ndovu-nyika (Loxodonta africana africana) na ndovu-misitu (Loxodonta cyclotis).

Tembo wa savanna wa Afrika, ndiyo tembo mkubwa kuliko wote. Ndiyo mnyama wa ardhini aliye mkubwa kuliko wote, huku tembo dume akiwa na urefu wa mita 3.2 mpaka 4 mabegani na uzito wa kg. 3,500 mpaka 12,000. Tembo jike huwa mdogo kiasi huku wengi wakiishia urefu wa mita 3 tu.

Wengi wa tembo wa savanna wa Afrika hupatikana katika nyika, mabwawani, na kwenye fukwe za ziwa. Hukaa sana kwenye kanda za savanna kusini mwa jangwa la Sahara.

Spishi nyingine ya ndovu wa Afrika ni ndovu-misitu (Loxodonta cyclotis), ambao ni wadogo na wa mviringo kiasi, pembe zao zikiwa fupi kiasi na zilizonyooka kuliko tembo wa savanna. Tembo wa misituni hufikia mpaka uzito wa kg. 4500 na husikia urefu wa mita 3. Mambo mengi hayafahamiki kuhusu tembo hawa ukivilinganisha na tembo wa savanna, kutokana na mazingira wanamoishi. Mara nyingi huishi katika misitu ya Afrika, ile mizito nay a mvua, ya kati na magharibi mwa Afrika. Japo mara chache husogea mipakanai mwa misitu yao, na kuzaliana na tembo wa savanna.

Tembo wa Asia

[hariri | hariri chanzo]
Ndovu wa Asia

Tembo wa Asia ni mdogo kuliko tembo wa Afrika, ana masikio madogo, na kwa kawaida ni tembo dume tu ambao ndio huwa na pembe tu.

Ndovu wa Asia anazoea wanadamu, kwa hiyo katika nchi kama Uhindi au Uthai hutumiwa kama mnyama wa kazi akibeba mizigo au watu. Zamani spishi hii ilitumiwa hata vitani. Kwa mfano jemadari Hanibal wa Karthago alishambulia Dola la Roma kwa msaada wa ndovu wa kijeshi waliovuka milima ya Alpi.

Tembo wa Asia duniani, pia hufahamika kama tembo wa India, hukaribia 60,000 walau mara moja ya kumi ya tembo wa Afrika. Kwa ukaribu zaidi inakadiriwa kuwa tembo 38,000 mpaka 53,000 wapo misituni na 14,500-15,300 wanafungwa kwenye makazi ya watu nap engine 1000 hivi wametawanyika kwenye sehemu za kuonyeshea wanyama. Kupungua kwa tembo wa Asia, pengine ni kwa hali ya juu zaidi kuliko kwa tembo wa Afrika kutokana na ujangili na uvamizi wa makazi ya tembo unaofanywa na binadamu.

Tembo wa savanna

[hariri | hariri chanzo]

Hawa tembo wa Savanna (Elephas maximus sumatramus), wanapatikana tu hasa Sumatra, na ni wadogo kuliko wale wa India. Tembo hawa wana idadi takribani 2100 mpaka 3000. Wana rangi nyepesi ya kijivu kuliko tembo wengine wa Asia, na madoa ya pinki kwenye masikio yao. Tembo wa Sumatra huwa na urefu wa mita 1.7-2.6 mabegani mwao na uzito wao ni takribani kg. 3000

Viungo vya nje

[hariri | hariri chanzo]
Makala hii kuhusu mnyama fulani bado ni mbegu.
Je, unajua kitu kuhusu Ndovu kama uainishaji wake wa kibiolojia, maisha au uenezi wake?
Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari.
Simple English Wiktionary
Simple English Wiktionary
Wikamusi ya Kiswahili ina maelezo na tafsiri ya maana ya neno:
Simple English Wiktionary
Simple English Wiktionary
Wikamusi ya Kiswahili ina maelezo na tafsiri ya maana ya neno:

Ili kupata maelezo kuhusu masanduku ya uanapwa ya spishi angalia: Wikipedia:WikiProject Mammals/Article templates/doc.