[go: up one dir, main page]

Nenda kwa yaliyomo

Majusi

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
Mamajusi walivyochorwa huko Ravenna (Italia), katika Basilika la Sant'Apollinare in Classe, mwaka 600 hivi.

Majusi (Kiing. magus, magi) ni mtaalamu wa nyota katika fani ya unajimu.

Historia ya neno

[hariri | hariri chanzo]

Neno la Kiswahili limetokana na Kiarabu مجوس majus lililopokewa kutoka Kiajemi cha kale magâunô kupitia Kigiriki μάγος magos.

Kwa kuwa mara nyingi jina hilo linatumika katika wingi, linatokea ma-majusi; baadhi ya watu wakisikia au kusoma mwanzoni mwa neno silabi dabo ma-ma wanakuja kudhani ni wanawake, kumbe sivyo.

Kwa asili lilimaanisha makuhani wa dini ya Uajemi ya Kale, hasa wafuasi wa Zoroaster.

Wagiriki waliamini ya kwamba makuhani hao walikuwa na elimu ya siri hasa kuhusu nyota na utabiri wa nyota.

Kwa hiyo katika lugha kadhaa neno limeendelea kumaanisha ama wanajimu au watu waliojua maarifa ya ushirikina.

Matumizi yake ya kawaida leo

[hariri | hariri chanzo]

Leo kwa kawaida jina hilo linatumika kuwataja watu wa namna hiyo ambao kadiri ya Injili ya Mathayo (2:1-12)[1] walitokea mashariki kwa Israeli wakifuata nyota ya pekee ili kumfikia Mfalme wa Wayahudi aliyezaliwa, yaani Yesu.

Walipofika Yerusalemu kwenye ikulu ya Herode Mkuu walimfanya afadhaike kwa habari hiyo, lakini walielekezwa Bethlehemu kadiri ya utabiri wa nabii Mika.

Walifika na kumkuta mtoto Yesu akiwa na mama yake, Bikira Maria, wakamtolea zawadi: dhahabu, ubani na manemane.

Halafu wakaonywa wasimrudie Herode, bali warudi kwao kwa njia nyingine.

Kumbe Herode, alipoona hawarudi, akikusudia kumuua mtoto, aliagiza wauawe watoto wote wa kiume wenye umri chini ya miaka 2 katika eneo la Bethlehemu.

Liturujia ya madhehebu mbalimbali ya Ukristo inakumbuka ujio wa mamajusi kwa Yesu kama mwanzo wa maandamano ya watu wa mataifa wanaokuja kumuabudu.

Sikukuu husika inaitwa Epifania, yaani Tokeo (la Bwana kwa...).

Pia kuna sikukuu yao wenyewe, tarehe 24 Julai[2][3].

  1. 2:1 Yesu alizaliwa mjini Bethlehemu, mkoani Yudea, wakati Herode alipokuwa mfalme. Punde tu baada ya kuzaliwa kwake, wataalamu wa nyota kutoka mashariki walifika Yerusalemu, 2 wakauliza, "Yuko wapi mtoto, Mfalme wa Wayahudi, aliyezaliwa? Tumeiona nyota yake ilipotokea mashariki, tukaja kumwabudu." 3 Mfalme Herode aliposikia hayo, alifadhaika, yeye pamoja na wakazi wote wa Yerusalemu. 4 Basi akawaita pamoja makuhani wakuu wote na walimu wa Sheria, akawauliza, "Kristo atazaliwa wapi?" 5 Nao wakamjibu, "Mjini Bethlehemu, mkoani Yudea. Ndivyo nabii alivyoandika: 6 `Ewe Bethlehemu katika nchi ya Yuda, kwa vyovyote wewe si mdogo kabisa kati ya viongozi wa Yuda; maana kwako atatokea kiongozi atakayewaongoza watu wangu, Israeli."` 7 Hapo, Herode aliwaita faraghani hao wataalamu wa nyota, akawauliza wakati hasa ile nyota ilipowatokea. 8 Kisha akawatuma Bethlehemu akisema, "Nendeni mkachunguze kwa makini habari za mtoto huyo. Mkisha mpata nileteeni habari ili nami niende nikamwabudu." 9 Baada ya kumsikiliza mfalme, hao wataalamu wa nyota wakaenda. Kumbe ile nyota waliyokuwa wameiona upande wa mashariki iliwatangulia hata ikaenda kusimama juu ya mahali pale alipokuwa mtoto. 10 Walipoiona hiyo nyota, walifurahi mno. 11 Basi, wakaingia nyumbani, wakamwona yule mtoto pamoja na Maria mama yake; wakapiga magoti, wakamsujudia. Kisha wakafungua hazina zao, wakampa zawadi: dhahabu, ubani na manemane. 12 Mungu aliwaonya katika ndoto wasimrudie Herode; hivyo wakarudi makwao kwa njia nyingine.
  2. Martyrologium Romanum
  3. https://www.santiebeati.it/dettaglio/91510
Makala hii kuhusu mambo ya Biblia bado ni mbegu.
Je, unajua kitu kuhusu Majusi kama historia yake au athari wake?
Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari.