[go: up one dir, main page]

Walawi (Biblia)

ya tatu kitabu Biblia, mchanganyiko 27 sura ya
Pitio kulingana na tarehe 00:07, 5 Machi 2010 na VolkovBot (majadiliano | michango) (roboti Badiliko: an:Levitico)

Kitabu cha Walawi (pia: Mambo ya Walawi) ni kitabu cha tatu katika Biblia ya Kiebrania (Tanak) na katika Agano la Kale la Biblia ya Kikristo, kikifuata kile cha Mwanzo na kile cha Kutoka.

Kama vitabu vingine vyote vya Biblia, hiki pia kinatakiwa kisomwe katika mfululizo wa historia ya wokovu ili kukielewa kadiri ya maendeleo ya ufunuo wa Mungu kwa binadamu.

Majina

Katika lugha asili ya Kiebrania kinaitwa Wayikra (maana yake “Na aliita”) ambalo ni neno la kwanza katika kitabu hicho.

Kwa lugha ya Kiyunani, kinaitwa Levitikon (biblion), maana yake “(Kitabu cha) Walawi (au Makuhani)”. Kinaitwa hivyo kutokana na jina lake la Kigiriki katika tafsiri ya Septuaginta: "Λευιτικóς (levitikos - Cha Kilawi)".

Wengine wanakiita Kitabu cha Tatu cha Musa (au Mose) kwa vile inafikiriwa kuwa ndiye mwandishi wa kitabu hicho.

Yaliyomo

Katika masimulizi ya kitabu ni Musa anayepokea maagizo ya Mungu akisikia sauti yake kutoka katika hema ya kukutania. Maagizo haya yanahusu hasa ibada zinazoendeshwa katika hema la kukutania na baadaye amri hizi zilitumiwa kwa ajili ya ibada kwenye hekalu la Yerusalemu.

Kwa jumla hakisemi mengi kuhusu maagizo kwa Walawi wenyewe bali juu ya kazi ya makuhani ambao wote walitoka katika ukoo wa pekee wa kabila la Walawi.

Kitabu cha Walawi kina sura ishirini na saba, na sura zote zinahusu amri na maagizo ya Mungu kwa Wanaisraeli hasa sheria za ibada zenye kulenga utakatifu wa makuhani na wa sadaka.

Maagizo hayo yanaeleza sadaka (sura 1-7), walivyowekwa wakfu makuhani wa kwanza, yaani Aroni (au Haruni) na wanawe (sura 8-10), utakaso (sura 11-15), siku kuu ya msamaha wa dhambi (sura 16), na maagizo mbalimbali kuhusu maisha ya kila siku na uendeshaji wa ibada (sura 17-27).

Kadiri ya kitabu hicho, watu wa kabila la Lawi tu ndio walioruhusiwa kushughulikia ibada, tena kati yao ukoo wa Haruni tu ndio makuhani kamili kwa sababu Musa aliwateua Aroni na wanawe kwa huduma hii (Law 8,6-13). Ukuhani wa ukoo wa Aroni ukaitwa "ukuhani wa kilawi" kwa sababu walitoka katika kabila hili.

Kutokana na kazi hiyo Walawi hawakupewa sehemu ya nchi takatifu, ila Mungu mwenyewe ndiye fungu lao. Lakini taifa lote lilitakiwa liwe takatifu kutokana na uhusiano wake na Mungu (Law 19:1). Polepole maana ya utakatifu huo ilizidi kueleweka si kukwepa unajisi wa kiibada tu, bali unategemea hasa mwenendo mwadilifu.


Muhtasari

  • 1:1-7:38 Sadaka mbalimbali
  • 8:1-10:20 Kuthibitishwa kwa Ukuhani
  • 11:1-15:33 Usafi na unajisi
  • 16:1-17:16 Damu ya upatanisho
  • 18:1-22:33 Utakatifu katika maisha ya kila siku
  • 23:1-27:34 Matukio maalumu

Viungo vya Nje

Vitabu vya Agano la Kale

Mwanzo * Kutoka * Walawi * Hesabu * Kumbukumbu * Yoshua * Waamuzi * Ruthu * Samueli I * Samueli II * Wafalme I * Wafalme II * Mambo ya Nyakati I * Mambo ya Nyakati II * Ezra * Nehemia * TobitiDK * YudithiDK * Esta * Wamakabayo IDK * Wamakabayo IIDK * Yobu * Zaburi * Methali * Mhubiri * Hekima DK * SiraDK * Wimbo Bora * Isaya * Yeremia * Maombolezo * BarukuDK * Ezekieli * Danieli * Hosea * Yoeli * Amosi * Obadia * Yona * Mika * Nahumu * Habakuki * Sefania * Hagai * Zekaria * Malaki

Alama ya DK inaonyesha vitabu vya deuterokanoni visivyopatikana katika matoleo yote ya Biblia.