[go: up one dir, main page]

Nenda kwa yaliyomo

Uvumba

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
Gramu 100 za utomvu mkavu wa uvumba.
Uvumba kutoka Yemen.

Uvumba (pia: ubani) ni utomvu mkavu (uliokauka) wenye harufu ya kupendeza ukichomwa. Unapatikana kutoka miti ya aina Boswellia thurifera (pia: Boswellia sacra).

Matumizi ya kidini

[hariri | hariri chanzo]

Matumizi yake ni katika ibada za kidini lakini pia nyumbani.

Mataifa ya kale ya Mashariki ya Kati yalitumia uvumba mahekaluni kwa mfano Wamisri, Wayahudi na Waroma wa Kale.

Kutoka kawaida ya Uyahudi, lakini pia ya Dola la Roma, matumizi yake yameingia katika Ukristo na katika liturujia za Kanisa Katoliki na Kanisa la Kiorthodoksi.

Waprotestanti huwa hawaitumii isipokuwa sehemu za Waanglikana na Walutheri wenye mwelekeo wa kukazia urithi wa kiliturujia.

Matumizi ya kiganga

[hariri | hariri chanzo]

Kuna pia matumizi kama dawa ya kumeza kwa kusudi la kuimarisha akili na kumbukumbu lakini pia kwa kupambana na ugonjwa wa jongo.

Wamisri wa Kale waliitumia kwa kutunza maiti ya marehemu.

Biashara ya uvumba

[hariri | hariri chanzo]

Miti ya Boswellia hustawi katika maeneo yabisi kama Yemen, Omani, Somalia, Ethiopia na sehemu za Bara Hindi mbali na nchi zenye rutuba nzuri na watu wengi. Hivyo uvumba ulitafutwa sana na kufanyiwa biashara kama bidhaa ya thamani.

Katika taarifa za Injili ya Mathayo (kitabu cha Biblia ya Kikristo) uvumba ulikuwa kati ya zawadi zilizoletwa na mamajusi wa mashariki huko Bethlehemu kama zawadi kwa mfalme wa Wayahudi aliyezaliwa.