[go: up one dir, main page]

Nenda kwa yaliyomo

Ifakara

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
Ifakara kutoka ndege.

Ifakara ni kata na makao makuu ya Wilaya ya Ifakara Mjini katika Mkoa wa Morogoro, Tanzania na kitovu cha eneo lenye mashamba makubwa ya miwa. Postikodi namba katika Misimbo mipya ya posta ni 67501. Kuna kituo muhimu cha TAZARA.

Mji uko katika bonde la mto Kilombero takriban kilomita 420 kusini-magharibi mwa Dar es Salaam.

Ifakara ni mji mkubwa, wenye makabila makuu mawili maarufu kama Wapogoro na Wandamba, wenye mfanano wa kuelewana katika baadhi ya matamshi ya lugha zao.

Wakati wa sensa iliyofanyika mwaka wa 2012, kata ilikuwa na wakazi wapatao 55,956 [1] walioishi humo. Katika ile ya mwaka 2022 walihesabiwa 13,367 ila kwa wilaya nzima ni 290,424 [2].

Taasisi muhimu mjini ni Taasisi ya Afya Ifakara (Ifakara Health Institute) inayofanya uchunguzi wa kisayansi wa magonjwa kama malaria na ukimwi. Kanisa Katoliki linaendesha Hospitali ya St Francis inayotarajiwa kuwa hospitali ya wilaya pamoja na chuo cha wauguzi.

Tangu tarehe 14 Januari 2012 mji ni makao makuu ya Jimbo Katoliki la Ifakara.

Jina na historia

Jina Ifakara lilitokana na neno ufwakara lenye maana amekwishakufa.

Ni kwamba hapo zamani, mnamo miaka ya 1860, mji huo ulijulikana kwa jina la Making'inda. Making'inda alikuwa jumbe wa kabila la Wahehe aliyewekwa ili kulinda eneo hilo lililokuwa chini ya utawala wa Wahehe chini ya kiongozi wao mkuu Muyugumba. Kwa maana hiyo, basi, asili ya mji wa Ifakara ni ya Wahehe.

Kiongozi wa kwanza wa Wambunga kuingia kwenye mji huo alikuwa Lipangalala. Alipofika alikuta kuna ngome kubwa ya mtawala Making'inda. Ujio huo wa Lipangalala kwenye nchi ya Wahehe ulimchukiza Making'inda hata kufikia hatua ya kumuua moja ya watoto wa Lipangalala. Kitendo hicho kilimfanya Lipangalala kuwa na hofu ya watu wake, hivyo akawaagiza Wambunga wenzake walioko Ulanga kuja kukaa naye ili kuongeza nguvu ya jeshi lao. Mara kwa mara Making'inda alikuwa akiandaa vikosi vya Wahehe kuwavamia Wambunga. Ndipo vita vilipoanza baina yao. Wahehe walifanikiwa mara kadhaa kuwashinda vita Wambunga na kuwafukuza kabisa kwenye mji huo. Wambunga walikimbilia Migude na hata ng'ambo ya mto Kilombero. Hata hivyo Wambunga wakawa kimya kwa muda wakijipanga kwa uvamizi wa ghafla dhidi ya Wahehe. Hivyo ghafla siku wakawavamia na kuwaua, huku baadhi yao wakakimbilia milima ya Vidunda na katika uvamizi huo walifanikiwa kumuua Making'inda mwenyewe. Tangu hapo Wambunga wakatoka mafichoni wakaitawala nchi ya Making'inda,

Baadaye wamisionari wa Kidachi wakaingia miaka ya 1890 wakitambua majina ya maeneo kutokana na tawala za viongozi wa makabila, hivyo walipokuwa wanawauliza Wambunga kuhusu jina la mwenye mji Wambunga hawakutaka kulitaja jina la Making'inda, adui yao, isipokuwa wakawajibu kwa matamshi ya Kingoni kuwa "Afwilekala" wakimaanisha kuwa mwenyewe amekwishakufa tayari. Wadachi walishindwa kutamka neno Afwilekala ndipo katika matamshi yao likazaliwa jina IFAKARA. Hiyo ndiyo asili ya jina la mji huu wa Ifakara kwa mujibu wa kitabu cha Historia ya Wambunga.

Kwa maelezo ya wengine neno hilo lilihusu nyoka mkubwa ambaye alikuwa tishio kubwa kwa wakazi wa mji huo: watu mbalimbali waliuawa na mifugo pia kuuawa. Jitihada nyingi zilifanyika kumuangamiza nyoka huyo na mwishowe walifanikiwa kumuua, ndipo neno ufwakara lilipovuma kwamba amekwishakufa. Wageni wengi kutoka sehemu tofautitofauti walishindwa kutamka vizuri jina hilo wakatamka Ifakara, na mpaka leo ndilo jina kuu la mji huo. Inawezekana "nyoka" ilikuwa tu namna ya kumtaja kifumbo mtawala huyo wa kutisha.

Picha

Marejeo

  1. "Sensa ya 2012, Morogoro - Kilombero DC" (PDF). Ilihifadhiwa kwenye nyaraka kutoka chanzo (PDF) mnamo 2004-01-02. Iliwekwa mnamo 2016-06-03.
  2. https://www.nbs.go.tz

Viungo vya nje

Kata za Wilaya ya Ifakara Mjini - Mkoa wa Morogoro - Tanzania

Ifakara | Katindiuka | Kibaoni | Kiberege | Kidatu | Kisawasawa | Lipangalala | Lumemo | Mang'ula | Mang’ula 'B' | Mbasa | Michenga | Mkula | Mlabani | Msolwa Station | Mwaya | Sanje | Signal | Viwanjasitini


Makala hii kuhusu maeneo ya Mkoa wa Morogoro bado ni mbegu.
Je unajua kitu kuhusu Ifakara kama historia yake, biashara, taasisi zilizopo, watu au utamaduni?
Labda unaona habari katika wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari.
Tafadhali usiingize majina ya maafisa na viongozi wa sasa maana wanabadilika haraka mno.