Hatua ya mwanga
Hatua ya mwanga ni ya pili kati ya tatu za safari ya maisha ya Kiroho kadiri ya waandishi wengi, hasa wa Kanisa Katoliki.
Hatua inayotangulia ni ile ya utakaso na inayofuata ni ile ya muungano. Hatua ya mwanga ni mwendelezo wa ile ya utakaso, lakini inadai mwendo wa kasi zaidi.
Tukisafiri njia ileile moja, tunaweza tukaona mandhari mbalimbali: sehemu tambarare na mpando pengine mkali; tena tunaweza tukaipitia njia hiyo usiku au mchana, kukiwa na jua au mvua. Ni vivyo hivyo upande wa roho. Halafu tukisafiri kwa garimoshi hatuwezi kuharakisha tusisimame vituoni, wala kusimama kirefu. Hata katika njia ya Mungu kutaka kuwahi mno kunahatarisha maendeleo halisi ya hatua kwa hatua, lakini kusimama mno kunachelewesha, jambo baya vilevile kwa sababu kutosonga mbele ni kurudi nyuma.
Inafaa kueleza hatua ya mwanga kwa mpangilio ufuatao:
- kuingia hatua hiyo: kumeitwa uongofu wa pili au, kwa usahihi zaidi, kutakaswa hisi;
- sifa kuu za hatua ya wanaoendelea;
- ustawi wa maadili ya kiutu;
- ustawi wa maadili ya Kimungu;
- vipaji vya Roho Mtakatifu katika wanaoendelea, usikivu wao kwake na umakinifu wa kudumu zaidi;
- ongezeko la mwanga rohoni kwa njia ya ekaristi;
- sala ya kumiminiwa ya wanaoendelea na hatua zake;
- kasoro za wanaoendelea; haja ya kutakaswa roho ili waingie hatua ya muungano.
Ni kwamba inafaa tuzingatie ustawi wa maadili na vipaji kabla ya maendeleo ya vitendo vyake, ili kuonyesha vitendo bora vilivyo lengo la ustawi huo. Tena inafaa kufuata njia hiyo ya kupanda, tukizingatia kwanza ustawi wa maadili ya kiutu, halafu ule wa maadili ya Kimungu[1], halafu ule wa vipaji vinavyokamilisha maadili[2], hatimaye neema za mwanga, upendo na nguvu tunazotolewa kila siku katika ekaristi. Hivyo tutavumbua kuwa kwa kawaida sala ya wanaoendelea ni ya kumiminiwa. Kama tungeeleza kwanza sala, labda tungeieleza jinsi ilivyo katika watu ambao wanaonekana tu kuendelea, kumbe hawaendelei vya kutosha, badala ya kuieleza inavyotakiwa kuwa katika hatua hiyo ya mbele. Tutapanda juu kuelekea muungano na Mungu, yaani tutaona mambo kadiri ya safari ya mtu anayeendelea kutekeleza lengo lake.
Kuingia hatua ya mwanga
[hariri | hariri chanzo]Mara nyingi Biblia inawakumbusha waadilifu haja ya kumuongokea Mungu zaidi. Yesu aliwaambia waliomfuata tangu mwanzo, “Amin, nawaambia: Msipoongoka na kuwa kama vitoto, hamtaingia kamwe katika ufalme wa mbinguni” (Math 18:3), katika urafiki wa ndani na Mungu. Aliwahimiza watambue unyonge wao na jinsi wanavyomtegemea Baba wa mbinguni. Kwa namna ya pekee alisema na Mtume Petro kuhusu uongofu wake wa pili wakati wa mateso, “Simoni, Simoni, tazama, Shetani amewataka ninyi apate kuwapepeta kama vile ngano; lakini nimekuombea wewe ili imani yako isitindike; nawe utakapoongoka waimarishe ndugu zako” (Lk 22:31-32).
Liturujia inapokariri maneno juu ya uongofu haiwalengi tu wenye dhambi ya mauti wanaohitaji kuacha uovu waingie uadilifu, bali wengine pia ambao, pamoja na neema inayotia utakatifu, wana kasoro nyingi, hivyo wanahitaji kuongoka toka maisha ya Kikristo ya wastani kuingia maisha yenye juhudi: “Nirudieni mimi kwa mioyo yenu yote, na kwa kufunga, na kwa kulia, na kwa kuombolea. Rarueni mioyo yenu, wala si mavazi yenu, mkamrudie Bwana, Mungu wenu; kwa maana yeye ndiye mwenye neema, amejaa huruma, si mwepesi wa hasira, ni mwingi wa rehema, naye hughairi mabaya” (Yoe 2:12-13). Maneno ya namna hiyo yanamuelea mtu kadiri alivyoendelea Kiroho: ingawa ana neema inayotia utakatifu tangu miaka mingi, anajisikia kuhitaji uongofu kamili ili undani wenyewe wa utashi wake umuelekee Mungu tu. Aliyekwisha kulima anarudia ili plau iingie zaidi ardhini na kupindua udongo uzae iwezekanavyo. Kwa mtazamo huo walimu wa Kiroho wamesisitiza haja ya uongofu wa pili ili kuingia hatua ya mwanga ya wanaoendelea. [3] [4]
Kutakaswa hisi
[hariri | hariri chanzo]Uongofu wa pili, ambao tunaingia hatua ya mwanga, unaitwa na Yohane wa Msalaba “kutakaswa hisi” au “usiku wa hisi”. Mafundisho yake ni kama ifuatavyo.
“Kutakaswa hisi ni jambo la kawaida, linalowatukia wanaoanza walio wengi”. Baada ya jaribu hilo “wanaoendelea wapo katika hatua ya mwanga, ambapo Mungu analisha na kuimarisha roho… pasipo hiyo kuchangia kwa kazi au mawazo yoyote” ya makusudi. Inachotakiwa kufanya daima ni kuondoa vipingamizi na kuwa aminifu kwa neema. Madondoo hayo yanaonyesha katika hatua gani ya maisha ya Kiroho jaribu tunalolizungumzia linatukia kwa kawaida.
Haja ya kutakaswa hivyo
[hariri | hariri chanzo]Haja ya utakaso huo inatokana na kasoro za wanaoanza, zinazojumlishwa katika tatu: kiburi cha roho, ulafi wa roho na uzembe wa roho, ambamo tunakuta mabaki ya mizizi saba ya dhambi kama aina za upotovu wa maisha ya Kiroho. Ulafi wa roho ni kushikamana mno na faraja za kihisi ambazo pengine Mungu anajalia wakati wa sala, au ni kujifanya lengo la utume au la kazi nyingine. Kwa kawaida uzembe unatokana na kwamba, mtu asiporidhishwa alivyotaka kwa ulafi wa roho au aina nyingine ya umimi, anakosa subira na kukinai kazi ngumu ya kulenga utakatifu. Mara nyingi kiburi cha roho kinajitokeza ulafi wa roho au aina nyingine ya umimi vikipata vilivyotaka, au mambo yakienda mtu anavyotaka; hapo akitegemea ukamilifu wake, anahukumu vikali wengine, na kujifanya mwalimu: kumbe bado ni mwanafunzi maskini. Kiburi hicho kinasababisha unafiki fulani, jambo linaloonyesha kuwa yuko mbali na ukamilifu.
Pamoja na kasoro hizo anazo nyingine nyingi: udadisi unaopotosha adili la kupenda ukweli, kujiamini ambako anajithamini mno na kukasirika asipothaminiwa vile, wivu na kijicho vinavyosababisha masengenyo, njama na mashindano yanayodhuru jamii. Katika utume kasoro ya kawaida zaidi ni juhudi za kibinadamu tu ambazo anajifanya lengo, k.mf. kwa kuvuta watu kwake au kwenye kundi lake badala ya kuwavuta kwa Bwana. Hatimaye anafikiwa na majaribu, kushindwa au ajali; hapo anavunjika moyo, analalamika, anakunja uso, na kukosa hamu ya kujitahidi, mambo yanayotaka kuonekana kama unyenyekevu. Hayo yote yanaonyesha haja ya kutakaswa mpaka ndani.
Baadhi ya kasoro hizo zinaweza kurekebishwa kwa ufishaji tunaopaswa kujifanyia kwa nje na hasa kwa ndani; lakini huo hautoshi kung’oa mizizi iliyopenya akili, utashi n.k. “Mtu, kadiri ya nguvu zake, ajitahidi kujitakasa na kujikamilisha; hivyo atastahili neema ya kushughulikiwa na Mungu ambaye atamtakasa kutoka unyonge ule wote asioweza kuurekebisha peke yake. Kwa juhudi zake zote hataweza kamwe kufikia hatua ya kutakata kabisa kwa nguvu zake; zaidi tena hataweza kujiweka tayari kuungana na Mungu katika upendo kamili. Ni lazima Mungu mwenyewe aingilie kati na kumtakasa katika huo moto usioeleweka kwake, kwa namna tutakayosema. Ni lazima kwamba, sawa na daktari bora, atie chuma cha moto kwenye madonda yetu ili kukausha usaha na kansa”. Kwa maneno mengine ni lazima msalaba unaoletwa na Mungu ili kututakasa utimilize kazi ya ufishaji tunayojifanyia. Msalaba ndio unaofikisha kwenye mwanga wa uzima.
Hisi zinavyotakaswa
[hariri | hariri chanzo]Hali hiyo inabainishwa na dalili tatu: “Dalili ya kwanza ni kutoona faraja za kihisi katika mambo ya Mungu wala katika malimwengu… Bwana akitaka kutakasa hisi hatuachi tufurahie lolote. Ni dalili ya hakika kiasi kuwa ukavu huo na ukinaifu huo havitokani na makosa wala matendo mapungufu tuliyoyafanya hivi karibuni. La sivyo, umbile lingesikia mvuto au elekeo fulani kwa mambo yasiyo ya Mungu… Lakini, kwa kuwa ukinaifu kwa mambo ya mbinguni na ya duniani unaweza ukatokana na ugonjwa wa mwili au wa nafsi unaosababisha mtu asifurahie lolote, basi inahitajika dalili nyingine.
Dalili ya pili ya kutakaswa hisi ni kumkumbuka Mungu kwa juhudi na kuhangaika kwa kutomtumikia na kwa kurudi nyuma machoni pake, kwa sababu hatufurahii tena mambo ya Kimungu… Hangaiko la kutomtumikia Mungu likibaki ndani mwetu linaonyesha kuwa hali hiyo haitokani na uvuguvugu… Pengine inachanganyikana na shida ya nafsi; hata hivyo ukavu hautakosa kutakasa, ukiwa na hamu kubwa ya kumtumikia Mungu. Basi, mpaka hamu hiyo itakapodumu, hata kama hisi zina huzuni, mahangaiko na udhaifu katika utendaji kwa sababu hazivutiwi, roho inaendelea kuwa tayari na yenye nguvu…
Asili ya ukavu huo ni kwamba Mungu anaihamishia roho mema na nguvu vya hisi, na kwa kuwa hisi na umbile haviwezi kufyonza mema ya Kiroho, basi vinabaki na njaa, ukavu na utupu. Hakika hisi haziwezi kupokea yaliyo ya Kiroho tu. Upande wa roho, inayopata polepole lishe hiyo, inaimarika na kukesha na kuwa macho zaidi kuliko awali isimchukize Mungu. Isipofurahia toka mwanzo ladha na furaha ya Kiroho bali inaona ukavu na ukinaifu, ni kwa sababu ya upya wa badiliko… Kinywa cha roho hakijawa tayari wala kuzoea ladha mpya iliyo nyororo mno, kitakavyofanya hatua kwa hatua tu”. Kipindi hicho cha mpito kimefananishwa vizuri na watoto wanaoachishwa maziwa ili wapewe chakula kizito zaidi. Wanalilia ladha ya maziwa waliyonyimwa mpaka wazoee chakula kipya wanachopewa.
“Kiini cha lishe hiyo ni mwanzo wa kuzama katika mafumbo kwenye giza, ambako ni kukavu kwa hisi na kunabaki kumefichika na kwa siri hata kwa mhusika. Kwa kawaida anayeng’amua ukavu na utupu huo upande wa hisi anajisikia kutamani upweke na utulivu, asiweze kuwaza wala kutaka lolote maalumu. Kisha kufikia hatua hiyo, kama watu wa Kiroho wangejua kutulia tu… wangesikia wororo wa lishe hiyo ya ndani huku wamesahau yote… Lishe hiyo ni nyororo hivi kwamba kwa kawaida mtu akitaka kuionja, haionji kabisa… kama vile hewa isivyoshikika kwa mkono kufumbwa… Hapo mtu akitaka kutenda kwa uwezo wake anazuia kazi ya Mungu badala ya kuisaidia. Kazi ya Mungu inafanyika rohoni, wakati ukavu unapotawala hisi”. Hayo ni maendeleo ya kawaida ya maisha ya Kiroho, si jambo la pekee: mtu, ambaye alikuwa akitafakari kwa kupanga mawazo, anajisikia haja ya kutazama mambo ya Mungu kwa namna sahili, ya dhati, hai na ya kimapenzi zaidi; walau kwa kawaida hawezi tena kutafakari hivyo. Ni kama inavyomtokea mtoto aliyeanza kusoma hadithi: ukimnyang’anya hizo na kumrudisha kusoma alfabeti au silabisilabi, hawezi kwa sababu ameshapita hatua hiyo kwa kujifunza kusoma mfululizo. Maisha yanasonga mbele, hatuwezi kuyarudisha yalivyokuwa miaka iliyopita; ni vivyo hivyo upande wa roho.
“Ndipo inapotokea dalili ya tatu inayohakikisha ni hatua ya kutakaswa hisi. Ndiyo kushindwa kutafakari au kupanga mawazo kama awali kwa msaada wa ubunifu. Juhudi za kufanya hivyo hazizai lolote. Sababu ni kwamba Mungu anaanza kujishirikisha kwa mtu, si tena kwa njia ya hisi, wala kwa mifuatano ya mawazo ambayo inakumbuka na kupanga ujuzi, bali kwa njia ya roho tu, pasipo mifuatano ya mawazo, yaani Mungu anajishirikisha kwa tendo sahili la kuzama katika mafumbo”. Kisha kuingia hatua hiyo mtu anazidi kushindwa kutafakari kwa uwezo wake, ingawa pengine mwanzoni hali hiyo si ya mfululizo. “Katika hali hiyo Mungu anajishirikisha kwa mtu ambaye anabaki bila kutenda, kama vile mwanga unavyomfikia mwenye macho wazi asitende lolote kwa lengo la kuupokea. Basi, kwa mtu kuupokea hivyo mwanga wa kumiminiwa upitao maumbile ni kuelewa yote akibaki bila kutenda”.
Hivyo hali hiyo inajitokeza kwa dalili mbili mbaya (ukavu wa hisi na shida kubwa ya kutafakari kwa mpango), lakini iliyo muhimu na njema ni mwanzo wa sala ya kumiminiwa pamoja na hamu kubwa ya Mungu inayotokana nao. Ukavu na shida ya kutafakari vinatokana na kwamba neema inatwaa namna mpya, ya Kiroho tu, juu ya hisi na ya mifuatano ya mawazo inayotumia ubunifu. Bwana anaonekana kunyang’anya kitu (faraja za hisi), kumbe anatoa zawadi ya thamani zaidi: mwanzo wa sala ya kumiminiwa na upendo ulio wa Kiroho, safi na imara zaidi.
Sababu za hali hiyo
[hariri | hariri chanzo]Teolojia inaeleza hali hiyo ni utakaso maalumu ambao unatendwa na Mungu na kusababisha mwanzo wa sala ya kumiminiwa, ambao tena unasababisha hamu kubwa ya Mungu; tunaelewa hivyo kwa kuwa hatuwezi kutamani kwa nguvu lile lisilotuvuta. Hamu hiyo kubwa ya Mungu na ya ukamilifu inaeleza hofu ya kurudi nyuma (uchaji wa Mungu unaomtawala mtoto wake). Hatimaye ukavu wa hisi unaeleweka kwa kuwa neema inayotolewa hapo si ya kihisi bali ya juu: ni uvuvio maalumu wa Roho Mtakatifu, anayezidi kutokeza kazi yake kwa njia ya vipaji vyake.
Kipaji cha elimu kinaeleza dalili ya kwanza (kukosa faraja yoyote katika malimwengu na katika mambo ya Mungu yaliyofikiwa na hisi), kwa kuwa kinatufanya tung’amue utupu wa viumbe, yaani kasoro zilizomo ndani ya hivyo na ndani mwetu wenyewe. Ndiyo sababu kinahusiana na heri ya machozi yanayotokana na kujua uzito wa dhambi na ubatili wa viumbe: “Ubatili mtupu, ubatili mtupu, mambo yote ni ubatili” (Mhu 1:2; 12:8), isipokuwa kumpenda na kumtumikia Mungu.
Dalili ya pili inaonyesha kuwa katika hali hiyo vinajitokeza vipaji vya uchaji na nguvu pia. Tunakuta kwa namna wazi uchaji wa Mungu ambao ni kuogopa dhambi, si adhabu; uchaji huo unastawi pamoja na upendo, wakati hofu ya adhabu inapozidi kupungua. Kwa kipaji hicho mtu anashinda vishawishi vikali dhidi ya usafi wa moyo na ya subira, vinavyoendana mara nyingi na kutakaswa hisi. Kipaji hicho kinahusiana na heri ya maskini, wasiojidai walimu, bali wanaanza kupenda unyenyekevu wa maisha yaliyofichika ili wafanane zaidi na Bwana.
Katika hamu kubwa ya kumtumikia Mungu kwa vyovyote, inayodumu wakati wa ukavu, vishawishi na matatizo, kinajitokeza kipaji cha nguvu kinachohusiana na heri ya njaa na kiu ya haki ambayo Bwana anaisababisha na kuishibisha ndani mwetu. Katika hali ngumu, kipaji hicho kinakuja kusaidia maadili ya subira na ustahimilivu, umotomoto wa roho usije ukazimika kama ule wa hisi. “Kwa kipaji hicho mtu anataka kushinda kizuio chochote na kupita faraja yoyote, ili kumpata anayempenda” (Yohane Ruysbroeck). Ndio wakati wa kuelewa kwamba, “Ukiuchukua msalaba wako kwa radhi, utakuchukua wewe, utakuongoza mpaka mwisho unaotamani, yaani mwisho wa mateso yote; lakini siyo hapa duniani… Mara nyingine mtu hupata nguvu sana kwa kupenda masumbuko na pingamizi kwa ajili ya kutaka kufuata mfano wa Yesu msalabani. Hata mwisho asingependa tena kukosa mateso… Hiyo neema ina nguvu ya ajabu juu ya mwili dhaifu wa binadamu; inamwezesha kupokea kwa furaha na upendo mambo yote aliyozoea kuogopa na kuepa siku zote” (Kumfuasa Yesu Kristo II,12:5-8).
Hatimaye dalili ya tatu (shida kubwa zaidi na zaidi katika kutafakari) inatokeza kipaji cha akili: mwanzo wa sala ya kumiminiwa, ulio wa juu kuliko mifuatano ya mawazo inayotumia ubunifu, unaikata. Hapo mtu anapatwa na mtawanyo wa mawazo pasipo kuusababisha: ni kwamba ubunifu usipokuwa na kazi maalumu unatawanyika kwa kiasi fulani, wakati akili na utashi vinapozidi kuzama katika mafumbo. Ubunifu hautawanyiki hivyo tunaposoma au kutangaza Neno, la sivyo tungekwama. Kumbe unatawanyika inapoanza sala ya kumiminiwa, ambayo haitegemei mifuatano ya mawazo wala kutumia mlolongo wa picha akilini, hivyo ubunifu unabaki hauna kazi kwa kuwa hauwezi kujihusisha na jambo la Kiroho tu ambalo akili inalielekea kwa namna isiyo wazi. Mt. Yohane wa Msalaba alieleza huo “mwanzo wa sala ya kumiminiwa wenye giza na ukavu” ambapo Mungu anamlisha mtu, akimtakasa na kumjalia aache mifano na apenye maana ya matamko rasmi ya imani, ili kuufikia usahili mkuu ulio sifa ya mtu wa sala hasa. “Mwali wa kwanza wa kipaji cha akili unaumba rohoni usahili” (Yohane Ruysbroeck) unaoshiriki ule wa Mungu. “Kipaji cha akili kinafanya kazi ya kutakasa; kinatakasa roho kwa kuiinua juu ya picha za kihisi na juu ya udanganyifu” (Thoma wa Akwino). Hivyo kinatukinga na upotovu na kutufanya tusiishie maneno ya Injili bali tuifikie roho yake; kinaanza kutupenyeza vilindi vya mafumbo ya imani yanayotokezwa na matamko yake rasmi, ambayo yanakuwa hivyo kituo cha kwanza, si cha mwisho, cha ujuzi wetu. Kipaji cha akili kitafanya kazi hiyo hasa katika usiku wa roho, lakini kinaitokeza tangu wakati huu katika tendo la imani la kupenya linaloitwa la kumiminiwa kwa sababu haliwezi kufanyika pasipo uvuvio maalumu. Kwa njia hiyo yanaanza kutokea aliyoyaonyesha Mt. Thoma: “Ili mtu afikie usahili wa sala ya kumiminiwa, ni lazima akombolewe kutoka aina mbili za kukosa usahili, yaani ile inayotokana na tofauti za vitu… na ile ya mifuatano ya mawazo: hiyo inatokea vitendo vyake vinapounganika kutazama tu ukweli”.
Hali hiyo inatofautiana na uchovu wa nafsi kwa dalili ya pili na ya tatu. Hasa hamu kubwa ya Mungu na ya ukamilifu inaitofautisha na uchovu wa nafsi tu unaoweza ukawepo pamoja nayo.
La kufanya katika usiku wa hisi
[hariri | hariri chanzo]Ni vema usiku na mchana vipokezane katika maisha ya Kiroho kama katika maisha ya dunia; mradi tujue la kufanya katika vipindi hivyo tofauti, hasa giza likidumu muda mrefu kama katika kipindi tunachokiongelea.
Kwanza, Yohane wa Msalaba aliandika kwamba, hasa waliopo katika kipindi hicho cha mpito, “wanahitaji kiongozi anayeelewa hali yao, la sivyo watarudi nyuma, watapotea njia, wataangukia uvuguvugu au walau watachelewa kuendelea, waking’ang’ania kabisa kudumisha mbinu yao ya kutafakari na ya kupanga mawazo, au wakidai waonje faraja na kuridhisha vionjo vyao”. Wakati huo ni lazima wamuombe shauri kiongozi mwenye mwanga, kutokana na matatizo yanayozuka kisha kunyang’anywa faraja za kihisi, pamoja na ugumu wa kutafakari unaozidi kuwa mkubwa na vishawishi dhidi ya usafi wa moyo na subira ambavyo mara nyingi shetani anavizusha ili kumuondoa mtu katika sala.
Pili, “wanatakiwa kujipa moyo wakidumu kwa uvumilivu; wasihangaikie mateso yanayowapata, bali wamtumainie Mungu. Yeye hawaachi kamwe wale wanaomtafuta kwa moyo sahili na mnyofu; atawajalia neema za lazima kwa kufuata njia mpya na pengine atawainua kwenye nuru safi angavu ya upendo, akiwapitisha siku za mbele katika usiku wa pili, ule wa roho, kama ataona wanastahili”. Hakuna sababu ya kuvunjika moyo katika huo ukavu na utovu wa uwezo, sembuse ya kuacha sala kama kitu kisicho na faida. Kinyume chake, sala ina manufaa zaidi tukidumu kwa unyenyekevu na kujikana na kumtumainia Mungu. Ukavu wa hisi wa muda mrefu, pamoja na kuzidi kushindwa kutafakari, ni dalili ya uhai mpya wa juu zaidi. Kiongozi mwenye elimu na mang’amuzi, badala ya kusikitikia hali hiyo, anaifurahia. Kwa kuwa mtu anajikuta na haja yenye heri ya kutoridhika na vitendo vidogo vya imani, tumaini na upendo. Matendo mapungufu ya maadili hayo hayamtoshi tena; yanahitajika matendo ya juu na yenye kustahili zaidi. Tunakaribia pambazuko la hatua ya mwanga, inayostahili tuvuke kwa bidii usiku wenye giza unaoitangulia. Tunatakiwa kumtumainia Mungu anapotufanyia kazi chungu ya kututakasa mabaki ya mizizi saba ya dhambi yanayoathiri maisha ya Kiroho: je, tumkimbie daktari wa meno mara anapoanza kututia uchungu ili atuponye? Tusipotakaswa duniani kwa kustahili, tutakaswa toharani pasipo stahili.
Tatu, tusipoweza kutafakari tena kwa mifuatano ya mawazo, “tunapaswa kuridhika na mtazamo mtulivu wa kimapenzi kwa Mungu”. Kufanya juu chini ili turudi kutafakari kwa mifuatano ya mawazo ni kwenda kinyume cha mkondo wa neema badala ya kuufuata, hivyo ni kujichosha pasipo faida yoyote, ni kushuka tena, badala ya kukubali Mungu atuinue. Lakini inapowezekana, shida katika kutafakari zisipozidi ila zinajitokeza mara kadhaa tu, inafaa kurudia tafakuri sahili ya kimapenzi.
Nne, wenye ukavu wa muda mrefu wanaotaka faraja fulani, “waepe wasiwasi wowote, hamu kubwa au tamaa ya kuhisi uwepo wa Mungu ili kuridhisha mwonjo wao; kwa sababu madai hayo yote yanamvuruga tu mtu, yanamuondoa katika utulivu wenye amani, katika pumziko tamu la sala ya kumiminiwa anayoipata wakati huo… Ni kama mtu aliyepozi ili kuchorwa picha: akigeukageuka huku na huku kadiri anavyopenda, mchoraji anayechanganywa hivyo atawezaje kumaliza kazi yake? Kadiri mtu atakavyotafuta ladha na ujuzi wa kumridhisha, ataonja utupu usioweza kujazwa kamwe kwa njia hiyo”. Kwa maneno mengine, kutenda kibinadamu kwa kujifanya lengo, kinyume cha vipaji vya Roho Mtakatifu, unazuia uvuvio wake mwororo. Tusitafute kuhisi zawadi ya Mungu katika sala, bali tuipokee kwa mikono miwili katika giza la imani na bila kukusudia faida. Baadaye furaha ya Kiroho itakuja kuungana na tendo la kumiminiwa la kusali na la kumpenda Mungu, lakini hatupaswi kuitafuta, ila kumtafuta Mungu mwenyewe, aliye bora kuliko zawadi zake.
Mtu aliyefikia kipindi hicho cha mpito akifuata kiaminifu hayo tuliyoyasema, basi, “utendaji wa akili na utashi unapokoma, hauvurugi tena mwanzo wa sala ya kumiminiwa na Mungu. Yeye anamhuisha kwa wingi mkubwa zaidi wa amani, na kumuandaa kuwaka moto wa upendo ambao unaletwa na sala hiyo ya kumiminiwa yenye giza na ya fumbo na ambao unaenea rohoni. Kwa kuwa sala hasa ni mmiminiko tu ambao Mungu anautia kwa siri, kwa amani na kwa upendo, tusipouzuia unaiwasha roho kwa upendo”. Hapo “mtu anatakiwa kuridhika na mtazamo wa upendo na utulivu kwa Mungu”, pamoja na ujuzi wa jumla wa wema wake usio na mipaka, kama vile mtoto mwema anapomuona tena mama yake mpendevu baada ya kumsubiri miezi. Hapimi mapendo yao kama anavyofanya mwanasaikolojia, ila anaridhika na mtazamo wa upendo, utulivu na undani ambao, katika usahili wake, unapenya kuliko utafiti wowote wa elimunafsia. Huo mwanzo wa sala ya kumiminiwa iliyounganika na upendo, tayari ni utekelezaji bora wa maadili ya Kimungu na ya vipaji vya Roho Mtakatifu, ni tendo la kumiminiwa la imani yenye kupenya ambapo, katika kimya cha sala, tunapata maana halisi ya yale tuliyoyasoma na tuliyoyatafakari mara nyingi katika Injili. Ndivyo inavyoanza kwa kawaida sala ya kumiminiwa, roho inapoinuliwa kwa Mungu juu kuliko hisi, ubunifu na mifuatano ya mawazo.
Hata hivyo, “anayeanza kumiminiwa sala hajaenda mbali na tafakuri ya mpango kiasi kwamba asiweze kuirudia pengine” asipojikuta chini ya uvuvio maalumu wa Roho Mtakatifu. Teresa wa Yesu alisema pia juu ya haja ya kukimbilia tafakuri sahili mwanzoni mwa sala ya utulivu: inafaa, basi, kuanza sala kwa kutafakari polepole Baba Yetu au kwa kuongea kitoto na mama Maria ili atufikishe kwenye urafiki wa ndani na Mwanae. Ni vema kukumbuka alivyojitoa mhanga kwa ajili yetu na anavyozidi kujitoa sadaka katika misa. Mtu anayefuata kwa uaminifu njia hiyo, atapokea mara kadhaa mwanga wa ndani utakaomuonyesha maana halisi ya mateso na ya ekaristi. Hivyo maisha ya Kiroho yanazidi kuwa sahili kadiri yanavyoinuka juu: ndilo sharti la kuangaza na kuzaa sana.
Majaribu ambayo kwa kawaida yanaendana na usiku wa hisi
[hariri | hariri chanzo]Kwa kawaida wakati wa kutakaswa hivyo kwa uchungu, vinaongezeka vishawishi dhidi ya usafi wa moyo na subira vinavyoruhusiwa na Mungu ili kuchochea itikio la nguvu la maadili hayo yenye makao katika hisi. Itikio hilo linakusudiwa kuyaimarisha, kuyafanya yatie mizizi mirefu na hivyo yazidi kutakasa hisi na kuzitiisha chini ya akili iliyoangazwa na imani. Ndiyo sababu katika usiku wa roho vitakuwepo vishawishi hasa dhidi ya maadili ya Kimungu yenye makao upande wa juu wa nafsi. Kwa wengi majaribu hayo si makali kama kwa wengine ambao yanawadokezea kwamba, wakiwa waaminifu, Mungu atawafikishia ukamilifu wa juu. Mapambano hayo yakieleweka hivyo yanaonekana muhimu na mazuri kweli: pasipo hayo tungeridhika na juhudi ndogo kuliko maadili tuliyo nayo.
“Mungu ni mwaminifu; ambaye hatawaacha mjaribiwe kuliko mwezavyo; lakini pamoja na lile jaribu atafanya na mlango wa kutokea, ili mweze kustahimili” (1Kor 10:13). “Huwapa nguvu wazimiao, humwongezea nguvu yeye asiyekuwa na uwezo… Wao wamngojeao Bwana watapata nguvu mpya, watapanda juu kwa mbawa kama tai” (Isa 40:29,31). Jaribu linatufunulia unyonge wetu na haja ya kupata neema ya Mungu, linatulazimisha kuiomba na kumtegemea yeye, si sisi tena, kama anavyofanya baharia katika dhoruba. “Ndugu zangu, hesabuni ya kuwa ni furaha tupu, mkiangukia katika majaribu mbalimbali; mkifahamu ya kuwa kujaribiwa kwa imani yenu huleta saburi. Saburi na iwe na kazi kamilifu, mpate kuwa wakamilifu bila kupungukiwa na neno” (Yak 1:2-4). Tena wakati huo tunaweza tukapotewa na mema kadhaa ya kidunia tuliyoyategemea mno (k.mf. mali, heshima au urafiki); hapo Mungu anaomba kwa ajili yake mapendo hayo makubwa tusiyowahi kupanga tumpe. Pengine anaruhusu ugonjwa tujifunze kuteseka na kwamba peke yetu hatuwezi kitu, bali tunahitaji neema zake kwa ajili ya mwili na ya roho vilevile.
Matokeo ya kutakaswa hisi
[hariri | hariri chanzo]Tukistahimili vema majaribu hayo, yatazaa matunda ya thamani, hasa ujuzi hai na wa dhati wa Mungu na wa nafsi yetu. “Mtu anayekosa faraja anapojikuta katika hali ya kudumu ya tabu, ukavu na ukiwa, anaanza kumiliki kweli adili bora la lazima la kujifahamu. Hapo anaelewa kuwa peke yake hafanyi, wala hawezi kufanya kitu, hivyo hajithamini kwa lolote wala hajiridhii kwa lolote. Hapo Mungu anamthamini zaidi”. Akijifahamu hivyo anahisi zaidi ukuu wa Mungu, wema wake usio na mipaka, thamani ya stahili za Yesu na ya ekaristi sadaka na chakula. “Hivyo katika giza la usiku wa hisi unazuka mwanga unaomuangaza juu ya unyonge wake na juu ya ukuu usio na mipaka wa Mungu”.
Katerina wa Siena alisema kuwa ujuzi wa Mungu na wa unyonge wetu ni kama nukta ya juu na ya chini ya duara inayozidi kupanuka. Ujuzi huo wa kumiminiwa kuhusu unyonge wetu ndio mwanzo wa unyenyekevu halisi, unaotufanya tutamani kutojulikana na kuhesabika si kitu ili Mungu awe yote. Upande wake, ujuzi wa kumiminiwa wa wema usio na mipaka wa Mungu, unasababisha upendo mkubwa, wenye bidii na usiojitafutia faida, kwa Mungu na kwa watu ndani mwake, tena tumaini kubwa katika sala.
“Hapo upendo wa Mungu unakua, kwa sababu mtu hatendi tena kwa kuridhisha hisi, bali kwa Mungu tu… Mara nyingi sana, asipotarajia kabisa na anapozingirwa zaidi na ukavu pande zote, Mungu anamshirikisha ghafla utamu fulani wa Kiroho, upendo safi kabisa, mianga ya akili miororo sana; na kila fadhili ya namna hiyo ina thamani na nguvu kubwa kuliko yale yote aliyoyaonja kabla ya hapo. Lakini ni kweli kwamba mwanzoni hawazi hivyo, kwa kuwa hiyo kazi ya Kiroho ya Mungu, wakati huo ni nyororo sana, hivyo haijulikani na hisi” (Yohane wa Msalaba).
Hapo tunatembea katika mchanganyiko maalumu wa mwanga na giza. Tunainuka juu ya giza la chini linalotokana na viumbe, udanganyifu na dhambi; na tunaingia katika giza la juu linalotokana na mwanga ulio mkali mno kwa macho yetu dhaifu: ndio uzima wa Mungu ambao mwanga wake haufikiwi na hisi wala akili peke yake. Lakini kati ya hayo mawili upo mwali wa Roho Mtakatifu, mwanzo halisi wa hatua ya mwanga. Ukiangazwa na mwali huo, upendo uliokuwa wa kimapenzi tu unakuwa na bidii za kutenda na kwa roho ya sadaka unazidi kujinyakulia nafasi ya kwanza ndani mwetu, na kutujaza amani ya kuwashirikisha wengine. “Yeye anifuataye hatakwenda gizani kamwe, bali atakuwa na nuru ya uzima” (Yoh 8:12).
Hatimaye tuangalie kuwa kutakaswa hisi kunajitokeza na kunavumiliwa kwa kiasi tofauti. Kwa wasiofanya bidii zaidi “mara nyingi usiku wa ukavu wa hisi unasimamishwa. Unajitokeza na kutoweka mara kadhaa; pengine kutafakari kwa mpango hakuwezekani, pengine ni rahisi… Hao hawamalizi kamwe kuziachisha ziwa hisi zao, waache kabisa kuzingatia na kufikiria lolote; wana neema hiyo kwa kwikwi tu… Kwa kuwa wanakwepa uchungu unaotakasa, Mungu haendelei kuwatakasa; wanataka kuwa wakamilifu bila kukubali kuongozwa kwenye njia ya majaribu yenye kukamilisha”.
Sifa kuu za hatua ya wanaoendelea
[hariri | hariri chanzo]Hali ya wanaoendelea inatakiwa kuelezwa kwa kusisitiza ujuzi na upendo wao kwa Mungu, na kwa kuzingatia tofauti zilizopo kati ya hatua hiyo na ile iliyotangulia, kama kati ya utoto na ujana.
Ujuzi wa Mungu katika hatua hiyo
[hariri | hariri chanzo]Katika hatua iliyotangulia sanasana mtu alikuwa anamjua Mungu kupitia kioo cha vinavyoonekana (viumbe, mifano ya Injili na vitendo vya ibada), pamoja na kujifahamu kijuujuu tu. Kumbe anayeendelea amepata kujifahamu zaidi akipitia kipindi kirefu cha ukavu. Kwa kufahamu hivyo unyonge wake, amekuja kumfahamu Mungu pia kama kwa mang’amuzi kupitia mafumbo ya wokovu aliyoyazoea. Akiwa mwaminifu, katika mafumbo hayo anavipita vile vinavyoonekana, ashike vile vya Kiroho, hasa thamani isiyo na mipaka ya stahili za Yesu. Kwake rozari si kukariri tu Salamu Maria, bali ni sala hai na shule ya kuzama katika mafumbo. Akiishi vizuri zaidi na zaidi rozari yake, atafikia kumtazama Kristo katika sala. Chini ya Yesu na Bikira Maria atazidi kuingia fumbo la ushirika wa watakatifu, na kuchochewa hamu ya utukufu wa Mungu na ya wokovu wa watu, pamoja na kutiwa upendo kwa msalaba, nguvu ya kuubeba, na pengine mwonjo fulani wa uzima wa milele kwa njia ya tumaini. Zaidi na zaidi atapenya na kuonja mafumbo ya imani na kuyaona katika uhusiano na maisha ya kila siku. Kadiri ya uaminifu wake atajaliwa kipaji cha akili kinachofanya imani ichungulie uzuri sahili na wa hali ya juu wa mafumbo hayo.
Ndiyo sababu hatua hiyo inastahili kuitwa ya mwanga. Katika ile iliyotangulia Bwana alijipatia hisi zetu kwa kuzijalia faraja, lakini kwa kuwa tulishikamana nazo mno ilitubidi tuachishwe hizo ili kupewa chakula cha Kiroho na cha nguvu zaidi. Sasa Bwana anajipatia akili yetu kwa kuihuisha, akiiangazia anavyoweza yeye tu na kuifanya izidi kuwa sikivu kwake ili ishike ukweli wa Kimungu. Mara nyingi mianga hiyo haitambulikani, lakini inazidi kutujulisha roho ya Injili, juu ya mahangaiko na fujo ya elimu ya kibinadamu tu. Inatufanya tutamani usahili mkuu wa mtazamo wa upendo unaotulia katika moyo wa Yesu aliye njia, ukweli na uzima. Hapo pana ujuzi wa Mungu na wa nafsi yetu ulio tofauti na ule unaopatikana kwa kusoma vitabu. Hivyo ni vya lazima kwa kufafanua Biblia, kutetea mafundisho ya Kanisa, kulinganisha maelezo ya wanateolojia. Lakini tusiishie maneno yake, bali hayo yawe mwanzo wa safari ya kung’amua fumbo lenyewe. Kwa imani tunazo tayari kweli tunazohitaji kuzijua; hivyo badala ya kujitafutia taarifa nyingi za kandokando tuziishi kweli hizo kwa kupokea kwa mikono miwili uvuvio wa Roho Mtakatifu. Si bure kwamba waadilifu wote wana vipaji saba, ambavyo kati yake kile cha akili kinakusudiwa kuwafanya wapenye maana na uzito wa matamko ya imani. Basi, inatokea kuwa wenye moyo safi na mnyofu wanayaona hayo kimaisha kuliko wanateolojia walioridhika na elimu waliyopata kwa kusoma.
Kinachoweza kuzuia tusizame katika mafumbo ni kujidai tunajua mengi, kumbe tunapaswa bado kujifunza mengi Kiroho. Kusoma vitabu hakutaweza kamwe kushika nafasi ya sala; ndiyo sababu walimu wa Kanisa walisema wamejifunza katika sala kuliko katika vitabu bora. Hivyo vinafafanua maneno, kumbe sala ya dhati inaipata ile roho inayoyahuisha, inaupata mwanga wa ndani unaoweza ukaangazia ghafla mawazo yaliyokaririwa bila kutambua yanavyohusu mengi katika maisha. Kwa mfano, “Una nini usichokipokea?” (1Kor 4:7) ndiyo msingi wa unyenyekevu, shukrani na upendo kwa Mungu ambaye alitangulia kutupenda na ndiye asili ya uhai, ya wokovu, ya neema na ya kudumu mpaka mwisho. Ndiyo namna ya kumjua anayohitaji mtu anayeendelea.
Upendo kwa Mungu na kwa watu katika hatua hiyo
[hariri | hariri chanzo]Mianga hiyo inatufanya tusimpende Mungu kwa kukimbia tu dhambi za mauti na zile nyepesi za makusudi (kama katika hatua iliyotangulia), bali kwa kuiga maadili ya Bwana (hasa upole na unyenyekevu) na kukwepa matendo mapungufu. Hapo, kwa wingi mkubwa zaidi na zaidi wa mianga ya ndani, tutapokea mara kadhaa hamu kubwa ya utukufu wa Mungu na ya wokovu wa watu, na urahisi mkubwa zaidi katika sala (si adimu sala ya kumiminiwa ya utulivu ambapo kwa kitambo utashi unatwaliwa na mvuto wa Mungu) na katika utume (kwa kufundisha, kuongoza na kuratibu mipango). Baadaye tutahitaji kutakaswa roho ili kikome kiburi chote kinachotokana na urahisi huo wa kusali na kutenda. Safari ni ndefu bado, lakini wakati huo roho inastawi, maadili yanakomaa na kutokeza upendo kwa Mungu na kwa watu usioishia miguso, bali ni wa matendo na ukweli.
Tanbihi
[hariri | hariri chanzo]- ↑ Maadili ya Kimungu yanamhusu Mungu aliye lengo letu kuu na kutufanya tumsadiki, tumtumainie na kumpenda kuliko yote, kumbe maadili ya kiutu yanahusu njia za kulifikia lengo hilo. Maadili ya kiutu yanaingiza unyofu wa akili katika utashi na hisi: chini ya busara, polepole haki inakuja kutawala utashi, na nguvu na kiasi zinakuja kutawala hisi. Zaidi tena, yakiwa chini ya imani, yanaingiza katika utashi na hisi mwanga wa neema, yaani kanuni ya maisha ya wana wa Mungu. Kwa mfano, adili la kiasi likiongozwa na busara tu halizingatii mafumbo ya imani (jinsi tulivyoinuliwa kwenye uhai upitao maumbile, tulivyoathiriwa na dhambi asili, uzito wa dhambi ya mauti, thamani ya upendo na urafiki na Mungu, ukuu wa wito wa kuwa wakamilifu kama Baba wa mbinguni). Kumbe likiongozwa na imani pia, linazingatia hayo yote na kulenga si tu tuishi kadiri ya akili, bali kama wana wa Mungu.
- ↑ Ili tueleze ustawi wa maadili unaotakiwa katika hatua ya mwanga, inafaa tukumbuke mfano wa jengo la Kiroho, ambamo ni rahisi kutambua mafundisho mengi ya Yesu na ya Mtume Paulo yalivyoelezwa na Augustino na Thoma wa Akwino waliposema juu ya uhusiano wa maadili na vipaji vya Roho Mtakatifu. Kwanza Bwana alituambia tunavyopaswa kujenga si kwenye mchanga, bali kwenye mwamba, halafu Mt. Paulo akaongeza kuwa mwamba ndiye Kristo, ambaye yote yajengeke juu yake. Basi, ili kupandisha jengo hilo tunapaswa kuchimba misingi hadi tukute mwamba wenyewe. Uchimbaji huo wa kina unamaanisha unyenyekevu ambao ni wa msingi kwa kuwa unakomesha kiburi, asili ya dhambi zote. Haitoshi tuchimbe juujuu tu; tukimruhusu, Bwana mwenyewe atafanya kazi hiyo kwa kututumia mambo yanayotuaibisha. Tunavyoona katika mchoro, nguzo ya kwanza ya jengo lote ni imani, kwa kuwa maadili mengine ya Kimungu yanaitegemea. Mbele yake ipo nguzo ya tumaini linalotufanya tumtamani Mungu na uzima wa milele tukitegemea msaada wake ili kuufikia. Juu ya nguzo hizo mbili linapanda paa la upendo, ulio adili bora; sehemu yake inayoelekea mbinguni inamaanisha upendo kwa Mungu, ile inayorudi nchini inamaanisha upendo wa kidugu unaotufanya tumpende jirani kwa ajili ya Mungu. Juu ya paa upo msalaba unaotukumbusha kuwa upendo wetu unatokana na stahili za Kristo na mateso yake. Kila adili la Kimungu linahusiana na kipaji kimojawapo cha Roho Mtakatifu kilichochorwa kama taa. Kwenye nguzo ya imani unapatikana mwanga wa kipaji cha akili, kinachofanya imani ipenye Neno la Mungu: k.mf. tukitaka kuchanganyikiwa na kishawishi, tunahisi kwamba Mungu ndiye lengo letu kuu, na kwamba tunatakiwa kudumu waaminifu kwake. Kwenye nguzo ya tumaini upo mwanga wa kipaji cha elimu ambacho tunajua mambo yanavyotokana na viumbe vyenye kasoro. Ndiyo sababu kinatuonyesha ubatili wa malimwengu na wa misaada ya kibinadamu katika kumlenga Mungu. Kwa maana hiyo kipaji hicho kinachokamilisha imani, kinakamilisha tumaini pia kwa kutufanya tutamani zaidi uzima wa milele na kutegemea msaada wa Mungu ili kuufikia. Tumaini linasaidiwa pia na kipaji cha uchaji kinachotukinga na kosa la kujiamini kipumbavu. Kwenye paa, linalomaanisha upendo, inaning’inia taa ya kipaji cha hekima ambayo inaangaza jengo lote na kutuonyesha yote yanavyotokana na Mungu, yaani na upendo wake au walau ruhusa yake inayokusudia jema kubwa zaidi (ambalo tutaliona kwa hakika mbinguni, lakini pengine kuanzia duniani). Katika jengo hilo anakaa Roho Mtakatifu pamoja na Baba na Mwana ili kujulikana na kupendwa. Ili kuliingia jengo ni lazima kupitia mlango ambao una bawaba nne, yaani maadili ya busara, haki, nguvu na kiasi. Pasipo hayo tunabaki nje, kwenye magugu ya umimi na ya maelekeo yasiyoratibiwa. Bawaba mbili za juu zinamaanisha busara na haki zilizopo upande wa juu wa roho, na bawaba mbili za chini zinamaanisha nguvu na kiasi zilizopo upande wa hisi. Kila bawaba ina ncha tatu zinazomaanisha maadili muhimu zaidi kati ya yale yanayohusiana nayo. Hivyo busara inategemeza utabiri (wa matokeo ya matendo), uchunguzi (wa hali tunapopaswa kutenda), na udumifu (tusije tukaacha kwa sababu ya magumu yanayokabili tuliyoyaazimia mbele ya Mungu baada ya kufikiri: kutodumu ni namna ya kukosa busara). Haki inategemeza maadili mengi; tutaje yanayomhusu Mungu: ibada inayompatia heshima inayotupasa, toba inayompa fidia ya makosa yanayomchukiza, na utiifu ambao tunatekeleza amri zake na za wawakilishi wake (wa Kiroho na wa kidunia). Nguvu inatudumisha kwenye njia njema kati ya hatari kubwa, badala ya kushindwa na hofu: vilevile inategemeza maadili mengine, hasa subira inayovumilia matatizo, moyo mkuu unaolenga kutenda makuu pasipo kukatishwa tamaa, na ustahimilivu unaotudumisha muda mrefu katika shida zinazojirudiarudia kila siku, pengine miaka na miaka. Hatimaye kiasi kinachoratibu hisi zetu, kinategemeza usafi wa moyo, upole unaoratibu hasira, na ufukara wa Kiinjili unaotufanya tutumie malimwengu bila kushikamana nayo. Kila adili-bawaba linahusiana na kipaji kimojawapo cha Roho Mtakatifu, kilichochorwa kama kito cha kupambia mlango. Busara inahusiana na kipaji cha shauri kinachotuangaza busara yenyewe inaposita. Haki inahusiana na kipaji cha ibada kinachotusaidia katika ukavu wa muda mrefu kwa kututia upendo wa kitoto kwa Mungu. Nguvu inahusiana na kipaji cha nguvu kilicho wazi katika wafiadini. Kiasi kinahusiana na kipaji cha uchaji wa Mungu kinachotufanya tushinde vishawishi vichafu: “Mwili wangu unatetemeka kwa kukucha wewe” (Zab 119:120). Hayo tuliyoyasema yanaweza yakaonekana kukosa usahili wa mambo ya Mungu, lakini tutauona tena kwa neno lifuatalo. Ikiwa mtu au jumuia fulani msingi na paa vya jengo lake ni kama vinavyotakiwa kuwa (yaani tunakuta unyenyekevu mkubwa na upendo halisi wa kidugu, ulio dalili kuu ya maendeleo katika kumpenda Mungu), basi yote yanakwenda sawa, kwa sababu hapo Mungu anafidia kwa vipaji vyake upungufu wa ubinadamu, na anakumbusha mfululizo wajibu akitoa neema ya kuutekeleza vema. “Mungu huwapinga wajikuzao, bali huwapa neema wanyenyekevu” (Mith 3:34; Yak 4:6; 1Pet 5:5) na hawaachi kamwe wanaoshika amri ya upendo: “Mpendane. Kama vile nilivyowapenda ninyi, nanyi mpendane vivyo hivyo. Hivyo watu wote watatambua ya kuwa ninyi mmekuwa wanafunzi wangu, mkiwa na upendo ninyi kwa ninyi” (Yoh 13:34-35).
- ↑ Kwa mfano, Alois Lallemant aliandika: “Kwa kawaida katika maisha ya walio wengi kati ya watakatifu na ya watawa wanaofikia ukamilifu, uongofu unatokea mara mbili: kwanza wanapojiweka wakfu kumtumikia Mungu, pili wanapojitoa kabisa kwa ukamilifu… Uongofu huo wa pili hautokei katika maisha ya watawa wote kwa sababu ya uzembe wao… Basi, tujipe moyo upya tusijihurumie katika juhudi za kumtumikia Mungu… Polepole juhudi zitakuwa tamu zaidi na matatizo yatapungua kwa sababu, kadiri moyo wetu utakavyozidi kutakata, tutapokea neema kwa wingi zaidi na zaidi”. Katika maisha ya watakatifu kuna kipindi cha tabu, kigumu kuvukwa, ambacho kinaingiza katika maisha ya juu zaidi na kuitwa “usiku wa hisi”, kikifuatwa na kingine kinachoitwa “usiku wa roho”. Ikiwa katikati ya vipindi hivyo unaonekana tayari ushujaa wa maadili (ambao unakuwa wazi zaidi baada ya kile cha pili), maana yake mtumishi wa Mungu amevuka vizuri hayo mahandaki yenye giza; hapo tabu hizo, badala ya kukanusha utakatifu wake, zinauthibitisha. Uwepo wa haja hiyo ni wazi kwa sababu wanaoanza wanajipendea hata baada ya miaka ya juhudi. “Sababu ya kuchelewa sana kufikia ukamilifu, au kutoufikia kamwe, ni kwamba katika mambo karibu yote tunafuata tu maumbile na busara ya kibinadamu. Tunakubali kidogo sana, au karibu hatukubali kabisa kuongozwa na Roho Mtakatifu, ambaye sifa yake ni kuangaza, kuelekeza na kutia moyo. Watawa walio wengi, hata walio wema na waadilifu, wanapojiongoza na wanapoongoza wengine, wanafuata tu akili na busara ya kibinadamu, ambayo wengi wao wanayo sana. Hiyo ni nzuri, lakini haitoshi kuufikia ukamilifu wa Kikristo” ambao unapita maumbile na kudai tutumie mara nyingi kipaji cha shauri. “Kwa desturi watu hao wanaongozwa na mitazamo ya kawaida ya watu wanaoishi nao; kumbe hao, hata kama hawavunji taratibu zilizopangwa, wako mbali sana na ukamilifu, kwa sababu idadi ya waliokamilika ni ndogo sana. Basi nao pia hawafikii kamwe vilele vikuu vya roho: wanaishi kama umati unavyoishi, na namna yao ya kuongoza wengine ina kasoro kubwa. Roho Mtakatifu anavumilia muda fulani, akisubiri wajirudi na, kisha kutambua rohoni mwao kazi tofauti za neema na za maumbile, wajiweke tayari kufuata uongozi wake. Lakini wakipoteza muda na fadhili anavyowajalia, hatimaye anawaacha peke yao katika giza la ujinga kuhusu hali yao ya ndani”. “Wokovu wa mtawa unafungamana moja kwa moja na ukamilifu wake, hivi kwamba akiacha juhudi za kuendelea Kiroho, anapiga hatua kuelekea maangamizi yake na kupotea milele. Asipofikia hapo ni kwa sababu Mungu, akitaka kumuokoa, anamkinga kwa huruma kabla hajatumbukia shimoni. Walimu wote wa Kiroho wanakubaliana kwamba, kutosonga mbele ni sawa na kurudi nyuma. Lakini watawa kadhaa, kwa kuwa wameshaendelea kiasi fulani, wanaishi pengine muda mrefu kidogo kabla hawajatambua kuwa wanarudi nyuma, kwa sababu hilo linatokea polepole”. “Kati ya watawa tunaweza kubainisha aina tatu tofauti. Wa kwanza ni wale wasiozikatalia kitu hisi zao. Wakiwa na baridi, wanaota moto. Wakiwa na njaa, wanakula. Wakipata wazo la kujiburudisha, wanafanya hivyo bila wasiwasi, wakilenga daima kujiridhisha hata wasijue kimaisha maana ya kujikatalia. Kazi zao wanazifanya kiofisi, pasipo roho, ladha wala tunda. Hao wako hatarini… Aina ya pili ya watawa inakwepa kufikia kiasi hicho ikijikatalia raha inazoziona kuwa si za lazima; lakini hao pia wanadanganyika kufuata kinachoonekana chema. Wanafanya mpango unaowapendeza, halafu wanatafuta visingizio vya uadilifu ili kupamba chaguo lao na kutetea mwenendo wao. Kazi zao wanazifanya kiaminifu kwa nje, lakini bila kujitahidi kwa ndani na kukusanya mawazo, wakiziacha hisi zao huru mno na kupuuzia utunzaji wa moyo. Watawa hao wamejaa matendo mapungufu na dhambi nyepesi… Aina ya tatu ni ya waliokamilika, ambao wameachana na tamaa yoyote, hawapendelei chochote, wanaridhika na yote na kutafuta tu matakwa ya Mungu. Hao wanafaulu kuunganisha utimilifu wa kushika taratibu za nje na juhudi kwa maisha ya ndani, wakikesha kwa kutunza moyo, wanadumisha amani ya roho na kutekeleza umakinifu kadiri utiifu unavyoruhusu. Watawa hao wanajaliwa fadhili tatu kubwa za Nafsi tatu za Utatu Mtakatifu: toka kwa Baba, nguvu ambayo karibu haishindiki katika utendaji, mateso na vishawishi; kwa Mwana, miali na miangaza ya ukweli inayong’aa mfululizo rohoni mwao; kwa Roho Mtakatifu, bidii, utamu na faraja za kushangaza”. Haja ya uongofu wa pili inatokana na mabaki yote ya umimi, ambao mara nyingi hautambulikani, lakini unachanganyikana na matendo yetu. Kwa wengi inatokana pia na kwamba hawataki kuonekana wajinga, wasitofautishe vya kutosha ujinga na ule unyofu wa hali ya juu unaotakiwa kustawi ndani mwao. Hivyo wanakuwa wanyofu na wakweli kidogo kuliko awali mbele ya Mungu, ya wakubwa wao na ya nafsi yao. Kwa kisingizio cha kutumia busara wanazingatia tu vipengele vidogo vya mambo makuu na kupuuzia wajibu wa kila siku katika mengi. Polepole, wakiacha unyofu wa mtazamo wa awali unaotakiwa kukamilika katika sala ya kumiminiwa, wanaangukia fujo ya mawazo yanayojidai kuwa ya hekima. Wanasahau kimatendo ukuu wa maadili ya Kimungu na umuhimu wa unyenyekevu. “Utawani kuna ulimwengu mdogo, ambao mambo yake ni: kujali vipawa vya umbile, kutamani kazi, nyadhifa na vyeo muhimu, kupenda na kutafuta ufanisi na sifa, raha na maisha ya starehe. Ndiyo mambo ambayo shetani anaundia tamasha lake la wanasesere ili kutuvuta na kutudanganya. Yeye anajua kuchezea vizuri mambo hayo yote mbele ya macho yetu hata tukasimama kuyatazama na kuchanganyikiwa nayo, tukipendelea madanganyifu hayo kuliko mema halisi ya kudumu”. Mara ngapi vipawa vya kibinadamu vinaheshimiwa kuliko maadili yapitayo maumbile! “Sala tu inaweza kutukinga dhidi ya udanganyifu huo. Yenyewe inatufundisha kupima mambo kwa hekima, yaani kuyatazama kwa mwanga wa ukweli, unaoondoa ono lake bandia na mivuto yake midanganyifu”. “Kwa siku moja tu tunatenda zaidi ya matendo mia ya kiburi” karibu bila kujitambua; lakini “maangamizi ya roho asili yake ni kuzidisha dhambi nyepesi, kunakosababisha kupungua kwa mianga na miongozo ya Kimungu, kwa neema na faraja za ndani, kwa bidii na moyo katika kupinga mashambulizi ya shetani”. Vipaji vya Roho Mtakatifu vinazuiwa na mshikamano wetu na dhambi nyepesi, vinakuwa kama tanga zilizokunjwa badala ya kupepea. Haitoshi tuelekeze baadaye nia yetu kwa Mungu ikiwa tendo letu ni la kibinadamu tu, na moyo wetu haujatolewa kweli kwake. Kujitoa kijuujuu hakutoshi, unahitajika uongofu mpya na halisi hata moyo umlenge kikamilifu. Matunda ya uongofu wa pili yanaelezwa na padri huyo katika mawaidha yake kwa wahubiri, “Wengine wanajichosha kabisa kusoma ili kutoa hotuba nzuri, na hata hivyo hawachumi karibu tunda lolote. Sababu gani? Ni kwamba kuhubiri ni kazi ipitayo maumbile kama vile lengo lake, yaani wokovu wa roho, na ni lazima chombo kilingane na lengo… Wahubiri wengi wana elimu ya kutosha, lakini si roho ya ibada na utakatifu vya kutosha. Njia halisi ya kupata elimu ya watakatifu na kuwa na mawazo ya juu… si kukimbilia vitabu, bali unyenyekevu wa ndani, usafi wa moyo, umakinifu na sala… Mtu anapofikia usafi kamili wa moyo, Mungu mwenyewe anamfundisha, mara kwa mpako wa faraja za Kiroho na wa nderemo za ndani, mara kwa mianga mitamu na ya kupendeza, ambavyo vinafundisha kuigusa mioyo ya wasikilizaji kuliko vinavyoweza kufanya masomo na mbinu nyingine za kibinadamu… Lakini hatufaulu kwa urahisi kuvua kiburi chetu na kujiachilia kwa Mungu... Mtu mwenye maisha ya Kiroho kweli atagusa mioyo kwa neno moja tu lililohuishwa na Roho wa Mungu, kuliko mwingine kwa hotuba nzima aliyoiandaa kwa kazi ngumu na kwa kumaliza nguvu zote za akili yake”.
- ↑ Mafundisho hayo yaliwahi kutolewa kwa namna nyingine na Katerina wa Siena, Henri Suso na Yohane Tauler, wote watatu Wadominiko wa Karne ya 14. Kadiri ya Katerina, Mungu alimuambia kuhusu upendo usiokamilika, “Kati ya wale ambao wamekuwa watumishi wangu wa ndani, baadhi wananitumikia kwa imani, pasipo hofu ya kitumwa: kinachowafanya waaminifu katika utumishi wangu si hofu ya adhabu tu, bali ni upendo. Lakini upendo huo haujakamilika, kwa kuwa katika kunitumikia wanajitafutia faida, yaani kile ambacho ndani mwangu kinawaridhisha na kuwapendeza. Upungufu huohuo umo katika upendo wao kwa jirani. Je, unajua dalili inayodhihirisha upungufu wa upendo wao? Ni kwamba wanaponyimwa faraja walizokuwa wakizipata ndani mwangu, upendo huo hauwatoshi tena, unafifia usiendelee kusimama. Unafifia, na mara nyingi unapoa zaidi na zaidi kwangu, ninapowaondolea faraja za Kiroho na kuruhusu badala yake wapatwe na mapambano na matatizo ili niwazoeshe katika uadilifu na kuwaondolea upungufu huo. Natenda hivyo kusudi tu niwasukume kwenye ukamilifu, na kuwafundisha wajifahamu vizuri na kujihakikishia kwamba wao si kitu, wala kwa wenyewe hawana neema yoyote… Kwa upendo wa namna hiyo usio kamili, ndivyo Mt. Petro alivyompenda Yesu mwema na mpole, Mwanangu pekee, alipofurahia kwa raha kabisa utamu wa urafiki wake wa ndani kwenye mlima Tabori... Lakini ulipofika wakati wa tabu, moyo wote ukatoweka. Si tu kwamba hakuwa na moyo wa kuteseka kwa ajili yake, bali alipopatwa na kitisho cha kwanza hofu ya kitumwa kabisa ikaja kushinda uaminifu wake, hata akamkana akila kiapo kwamba eti! Hajawahi kumfahamu… Ukamilifu wowote na adili lolote vinatokana na upendo, nao upendo unalishwa na unyenyekevu, ambao tena asili yake ni kujifahamu na kujichukia kitakatifu… Basi mtu anatakiwa ajizoeshe kung’oa takwa lake lolote… na kujifungia upwekeni ili kulia, kama alivyofanya Mt. Petro pamoja na wanafunzi wengine… Hata hivyo uchungu wa Petro ulikuwa haujakamilika, ukabaki hivyo siku arubaini zote na hata baada ya Bwana Kupaa, yaani mpaka Pentekoste iliyomaanisha kwa Petro na mitume wengine kuingia hatua ya waliokamilika”. Katika hali hiyo ya kumpenda Bwana kimamluki bado, mara nyingi maongozi yake yanatuachia sisi pia kosa fulani la wazi ili kutunyenyekesha na kutulazimisha kujirudi kama Mt. Petro pale Bwana alipogeuka “akamtazama”: basi, “akatoka nje akalia kwa majonzi” (Lk 22:61-62). Tuna sababu za kutosha tukahisi kwa umotomoto wa majuto yake hakurudishiwa tu kiwango cha neema alichopoteza, bali cha juu zaidi. Bwana aliacha aanguke kusudi aponywe kosa la kujiamini kipumbavu, awe mnyenyekevu zaidi na kumtegemea yeye tu. Kisha kuaibika na kulia kwa kosa lake akawa bora kuliko alipopanda Tabori hajafahamu udhaifu wake: alijinyenyekeza, akamshukuru Mungu kwa huruma yake isiyo na mipaka akaendelea hadi kifodini. Uongofu wa pili unaweza ukatokea pasipo kosa kubwa, k.mf. katika nafasi ya kuonewa au kusingiziwa ambayo, kwa neema ya Mungu, inachochea njaa na kiu ya haki badala ya mawazo ya kulipa kisasi. Katika nafasi ya namna hiyo, msamaha wa dhati unamvutia mtu neema nyingi zinazomuingiza kwenye hatua ya juu ya maisha ya Kiroho. Hapo anapata hisi mpya kuhusu mambo ya Mungu na juhudi asiyowahi kuwa nayo. Mtazamo wa ndani zaidi unaweza ukatokana pia na kufiwa mtu mpendwa, kufilisika, kushindwa vibaya na mengine yote yanayoonyesha ubatili wa malimwengu na umuhimu wa kile ambacho pekee ni cha lazima. Katerina alisisitiza haja ya kumuendea Baba kwa kumpitia Yesu msulubiwa: tuache kujifanya lengo la yote tukamtafute Mungu kweli tukifuata njia ya kujikana inayoleta amani ya ndani. Henri Suso alifundisha mengi kuhusu uongofu wa pili, alioung’amua baada ya miaka michache ya kuishi utawani kwa uzembe fulani. Ni muhimu hasa aliyoyasema juu ya watawa wanaozingatia mno masomo au taratibu za nje. Kwa mwanga wa Mungu aliona “aina hizo mbili za watu kuzunguka kandokando ya msalaba wa Mwokozi wasiweze kumfikia”, kwa sababu wanajifanya lengo la masomo au la utekelezaji wa taratibu za nje, na wanahukumiana pasipo upendo. Hapo akaelewa alivyopaswa kuzidi kujikana na kuwa tayari kupokea kwa upendo yale yote atakayotaka Mungu, pamoja na kutekeleza upendo mkubwa wa kidugu. Yohane Tauler aliyafananisha makundi hayo mawili na walimu wa sheria na Mafarisayo: “Walimu wa sheria walikuwa wasomi wanaojali sana ujuzi wao, kama vile upande wao Mafarisayo walivyojali sana ibada zao. Katika misimamo hiyo hakitatoka kamwe chochote chema. Ingawa ni adimu sana watu wasiokwama walau kiasi katika aina mojawapo au zote mbili za matope hayo, wengine wamekwama kuliko wenzao. Kwa jina la walimu wa sheria tuwaelewe… wanaodhani kujua mambo makuu. Ndipo wanapoweka utukufu wao wakitamka sentensi nzito wakati undani wao, unaotakiwa kububujika ukweli, unabaki tupu na mkavu. Upande wao Mafarisayo ni watu wa ibada wanaojiona bora na kujidhania kuwa kitu, wakishika sana ibada zao zote na taratibu zao kwa kudhani nje ya hizo hakuna jema lolote, na kwa kudai wasifiwe na kuheshimiwa kwa hizo. Undani wa roho yao umejaa lawama kwa wale wote wasiofanya sawa nao”. Tukikumbuka maneno ya Injili kuhusu sala ya Farisayo na ya mtozaushuru, tutaelewa haja yao ya kuongoka kwa ndani zaidi. Yohane Tauler alifafanua pia kiu ya Mungu ambayo inatokana na uvuvio wa Roho Mtakatifu, na kuendana na ukinaifu kwa viumbe vyote (yaani kwa fujo, uongo na ubatili wote vilivyonavyo), na mapambano dhidi ya maelekeo yasiyoratibiwa ya hisi. Jaribu hilo linafuatwa na kipindi cha pumziko na furaha, halafu mfululizo wa pili wa majaribu ambayo hatua ya waliokamilika inaanza. Ndiyo kazi ya Mungu hasa: kutakasa kwanza hisi, halafu roho, ili mtu aungane naye kwa dhati. Mwanzoni mwa uongofu wa pili Mungu anamwinda, naye pia anamtafuta, lakini kwa mapambano na mahangaiko. Hali hiyo inajitokeza kwa hamu kubwa ya Mungu na ya ukamilifu, na kwa mapambano “kwa sababu mwili hutamani ukishindana na roho, na roho kushindana na mwili” (Gal 5:17). Ndipo linapotokea hata fadhaiko la mtu kujiuliza kama ataweza kamwe kulifikia lengo analolitamani. “Mtu anapojikuta amezama katika hangaiko hilo na anapotambua Mungu anavyomwinda rohoni mwake, hapo bila shaka Yesu atafika na kuingia ndani mwake. Lakini asipotambua anavyowindwa wala asipohangaika hivyo, Yesu hafiki. Wasiokubali kushikwa na uwindaji huo na fadhaiko hilo, hawawi kamwe wema kweli. Wanabaki walivyo, hawarudi ndani mwao, na matokeo yake hawajui yanayotukia”. Tukipaswa kutaabika tupate digrii, hatupaswi kutaabika kidogo zaidi tuufikie ukamilifu. Kuna watu wanaodhani kuwa na hali hiyo, kumbe ni shida za nafsi; lakini pia si adimu watu ambao kweli wana hangaiko hilo, ila wakimkimbilia padri wapate mwanga wanajibiwa, “Usihangaike bure. Tulia tu: matakaso yanayozungumziwa na vitabu fulanifulani ni ya nadra na ya pekee”. Baada ya jibu hilo mtu haoni zaidi, tena anajisikia hajaeleweka. Basi, anayewindwa hivyo afanye “vile tu alivyofanya mwanamke Mkananayo: kumuendea Yesu na kumpazia sauti, yaani hamu kubwa, kwa kusema, Unirehemu, Bwana, Mwana wa Daudi! Lo, wanangu! Mungu kufukuza au kuwinda roho hivyo kunasababisha mlio wa dua wenye nguvu kubwa ajabu… kama kutoka vilindi visivyopimika. Huo unapita kabisa maumbile, kwa sababu ni Roho Mtakatifu mwenyewe anayetakiwa kuutoa ndani mwetu, alivyosema Mt. Paulo, ‘Roho mwenyewe hutuombea kwa kuugua kusikoweza kutamkwa’ (Rom 8:26)”. Hivyo mtu, ingawa anabaki mkavu, anaingia maisha ya kuzama katika mafumbo kwa uvuvio maalumu wa Roho Mtakatifu anayeanza hapo kutokeza kazi yake. Baada ya mlio huo, pengine Mungu anatenda kama Yesu kwa mwanamke huyo, akijifanya hasikii au hataki kusikiliza. Ndipo tunapopaswa kusisitiza, kama mama huyo alivyofanya vizuri ajabu kwa mwanga wa Mungu, aliyekuwa akimtafuta hata kwa makatalio na matusi bandia: “Jinsi hamu ya ndani ya roho inavyotakiwa kuwa kubwa na kali zaidi hapo!… Hata kama Mungu akikataa mkate, hata akikanusha hali yetu ya kuwa wana… tunatakiwa kumjibu kama vile Mkananayo, ‘Ndiyo, Bwana, lakini hata mbwa hula makombo yaangukayo mezani pa bwana zao’ (Math 15:27). Wanangu, tungefaulu hivyo kupenya undani wa ukweli… hapo Mungu au kiumbe chochote asingeweza kuwakanyaga nyinyi, kuwadhalilisha au kuwazamisha chini kiasi ambacho wenyewe msingejizamisha zaidi… mkitegemezwa na tumaini kamili, na juhudi kubwa zaidi na zaidi”. Ndivyo alivyofanya Daudi akitukanwa na Shimei (taz. 2Sam 16:5-14). “Ndio, wanangu, yote yanategemea jambo hilo, na atakayefikia hapo atafaulu kabisa. Njia hizo tu zinafikisha kweli kwa Mungu, pasipo kituo katikati. Lakini kwa bahati mbaya wengi wanaona haiwezekani kufikia kiwango hicho cha kujishusha moja kwa moja na kubaki chini kwa udumifu, kwa hakika halisi na kamili kama alivyofanya mama huyo. Ndiyo sababu akajibiwa, ‘Mama, imani yako ni kubwa! Na iwe kwako kama utakavy’o (Math 15:28). Hakika jibu hilohilo watapewa wale wote watakaopatikana na misimamo hiyohiyo kwenye njia hiyo”. Yohane Tauler alisimulia habari za msichana ambaye alijidhania kuwa mbali na Mungu, hata hivyo alijiachia daima katika matakwa yake matakatifu, limtokee lolote lile. Hapo “akainuliwa juu sana kuliko mshenga yeyote na kuvutwa kabisa ndani ya kilindi cha Mungu… Injili inavyofundisha, ‘Nenda ukaketi mahali pa nyuma’ (Lk 14:10) ndipo utakapopelekwa mbele zaidi. Lakini, ‘Kila ajikwezaye atadhiliwa’ (Lk 14:11). Uyatamani yale Mungu aliyoyataka tangu milele, upakubali mahali pale ambapo matakwa yake mapendevu yameamua pawe pako”. Pengine anataka katika mazingira yetu tuwe kama mzizi mdogo uliofichika ardhini, si ua linaloonekana na wote. Hata hivyo, kazi ya mzizi mdogo unaofyonza rutuba ya ardhi kwa kulisha mti ni kati ya zile za kufaa zaidi: heri wanaoshika nafasi hiyo vizuri! “Wanangu, ndivyo tunavyomuendea Mungu: kwa kujikana kabisa, kwa kila namna na katika yale yote tuliyonayo. Mtu anayeweza kupata tone moja tu la hiyo roho ya kujikana, anayepokea cheche yake moja tu, anajikuta tayari na kufikishwa karibu na Mungu kuliko kwa kuvua nguo ili kumpa jirani, au kwa kula mawe na miba kama umbile lingemruhusu. Nukta fupi ya kuishi kwa msimamo huo ingetufaa kuliko miaka arubaini ya vitendo vya kujichagulia”.
Marejeo
[hariri | hariri chanzo]- F. VAN VLIJMEN, W.F., Safari ya Kiroho, Mafundisho kwa Watawa (vitabu 2) – ed. T.M.P. Book Department – Tabora 1978
- R. GARRIGOU-LAGRANGE, O.P., Hatua Tatu za Maisha ya Kiroho, Utangulizi wa Uzima wa Mbinguni – tafsiri fupi ya Rikardo Maria, U.N.W.A. – ed. Ndugu Wadogo wa Afrika – Morogoro 2006
Viungo vya nje
[hariri | hariri chanzo]- "Ascetical Theology". Catholic Encyclopedia. New York: Robert Appleton Company. 1913.
- "Mystical Theology". Catholic Encyclopedia. New York: Robert Appleton Company. 1913.
- "Christian and Religious Perfection". Catholic Encyclopedia. New York: Robert Appleton Company. 1913.
- "Beatific Vision". Catholic Encyclopedia. New York: Robert Appleton Company. 1913.
- "Asceticism". Catholic Encyclopedia. New York: Robert Appleton Company. 1913.
- "State or Way (Purgative, Illuminative, Unitive)". Catholic Encyclopedia. New York: Robert Appleton Company. 1913.
- "Sanctifying Grace". Catholic Encyclopedia. New York: Robert Appleton Company. 1913.
- Ascetic theology from 1902 Catholic dictionary
Makala hii kuhusu dini ya Ukristo bado ni mbegu. Je, unajua kitu kuhusu Hatua ya mwanga kama historia yake, matokeo au athari zake? Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa? Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari. |