[go: up one dir, main page]

Nenda kwa yaliyomo

Firigogo

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
Firigogo
Firigogo wa Lichtenstein
Uainishaji wa kisayansi
Himaya: Animalia (Wanyama)
Faila: Chordata (Wanyama wenye ugwe wa neva mgongoni)
Ngeli: Aves (Ndege)
Oda: Pterocliformes (Ndege kama firigogo)
Familia: Pteroclidae (Ndege walio na mnasaba na firigogo)
Bonaparte, 1831
Ngazi za chini

Jenasi 2 na spishi 16:

Firigogo ni ndege wa nyika wa jenasi Pterocles na Syrrhaptes katika familia Pteroclidae. Wataalamu wengine wanawaainisha katika jenasi moja Pterocles. Wanafanana kidogo na njiwa lakini ni wanono kuliko hao.

Firigogo wana kichwa kidogo na shingo fupi kama zile za njiwa na mwili imara. Ukubwa wao unaenda kutoka urefu wa sm 24 hadi 40 na kutoka uzito wa g 150 hadi 500. Wapevu wana umbo tofauti kulingana na jinsia na madume ni wakubwa na wana rangi kali kuliko majike. Wana mabawa marefu yaliyochogoka na kila bawa lina manyoya makuu kumi na moja, na hii inawapatia mruko nyofu wa mbio. Misuli ya mabawa ina nguvu na ndege wanaweza kupeperuka haraka na kuendelea kwa muda. Katika spishi fulani, manyoya ya kati ya mkia yamerefuka na kuchongoka.

Miguu ni mifupi na wanajenasi wa Syrrhaptes wana manyoya yanayokua kwenyw miguu na vidole pia na hawana vidole vya nyuma, ilhali wanajenasi wa Pterocles wana miguu yenye manyoya mbele, hawana manyoya kwenye vidole na wana vidole vya nyuma visivyokamilika ambavyo vimeinuliwa ardhi. Manyoya yana rangi za kamafleji, k.m. rangi ya mchanga, kijivu na hudhurungi pamoja na madoa na/au milia, ambayo inawezesha ndege kulandana na mandhari ya vumbi. Kuna tabaka jembamba ya malaika ambalo husaidia kuhami ndege dhidi ya joto na baridi kali. Manyoya ya tumbo yamerekebishwa makusudi ili kufyonza maji na kuyahifadhi, ambayo inawezesha wapevu, madume hasa, kubebea makinda maji ambao wanaweza kuwa maili nyingi kutoka kwenye madimbwi ya maji. Kiasi cha maji kinachoweza kubebwa kwa njia hii ni ml 15 hadi 20.

Wanajenasi wa Syrrhaptes hupatikana katika mbuga baridi za Asia ya Kati. Msambao wao hutoka Bahari ya Kaspi kupitia kusini kwa Siberia, Tibet na Mongolia kuelekea kaskazini na kati ya Uchina. Kwa kawaida hukaa mahali pamoja lakini firigogo wa Pallas anaweza kuhama ndani ya eneo fulani na mara kwa mara huvamia na kuonekana katika maeneo mbali nje ya maeneo yake ya kawaida. Hii ilitokea miaka ya 1863 na 1888, na uvamizi mkubwa ulifanyika mwaka 1908 wakati ndege wengi walionekana mbali kama Eire na Uingereza ambako walitaga huko Yorkshire na Moray.

Wanajenasi wa Pterocles hupatikana hasa kwenye sehemu kavu za kaskazini, mashariki na kusini mwa Afrika ingawa msambao wa spishi fulani unaenea hadi Mashariki ya Kati na Asia ya Magharibi. Firigogo wa Madagaska anazuiwa Madagaska tu. Firigogo tumbo-jeusi na firigogo mkia-pini hutokea pia nchini Hispania, Ureno na kusini mwa Ufaransa. Takriban spishi zote hukaa mahali pamoja ingawa baadhi hufanya uhamiaji katika eneo fulani, kwa kawaida mpaka vimo vya chini wakati wa Majira ya baridi.

Lishe na kujilisha

[hariri | hariri chanzo]

Firigogo hula mbegu hasa. Lishe nyingine hujumuisha machipukizi na majani kijani, matunguu na beri. Wadudu kama vile sisimizi na mchwa huweza kuliwa wakati wa kuzaliana hasa. Lishe ya firigogo wengi ni ya kipekee na mbegu za idadi ndogo ya mimea zinatawala. Hii inaweza kutegemea upatikanaji wa mahali lakini katika visa vingine inaonyesha uteuzi halisi wa mbegu zilizopendekezwa kushinda nyingine na firigogo. Kwa kawaida mbegu za mimea ya aina za miharagwe ni sehemu muhimu ya chakula. Katika maeneo ya kilimo oti na nafaka nyingine huchukuliwa bila kusita. Mbegu zimekusanywa kutoka ardhi au moja kwa moja kutoka kwa mimea. Mbinu za kutafuta chakula hutofautiana kati ya spishi zinazoishi pamoja ambayo hupunguza ushindani; nchini Namibia firigogo mikufu-miwili hujilisha polepole na kwa kimbinu huku firigogo wa Namakwa hujilisha haraka wakichunguza udongo tifu kwa domo lao na kuufuta kando. Kokoto ndogo pia zinamezwa ili kusaidia kusaga chakula katika firigisi.

Firigogo hupenda kuwa pamoja na hujilisha katika makundi ya hadi ndege 100. Kama matokeo ya chakula chao kikavu, wanahitaji kutembelea vyanzo vya maji mara kwa mara. Wakati wa kunywa hutofautiana kati ya spishi. Spishi kumi hunywa alfajiri, nne alasiri na mbili kwa nyakati zozote. Wakinywa maji hufyonzwa ndani ya domo ambalo hufufuliwa halafu ili kuruhusu maji yatiririke ndani ya gole. Kwa kurudia utaratibu huu haraka maji ya kutosha kwa muda wa masaa ishirini na nne yanaweza kumezwa katika sekunde chache. Wanaposafiri kwenye madimbwi ya maji, huwaita ndugu wa spishi zao na mamia au maelfu wengi wanawashirikisha majilio yao kwenye mahali pa kunywa licha ya kutana kutoka maeneo mengi tofauti yanayotawanyika kwenye mamia ya kilomita mraba za maeneo.

Huwa rahisi kushambuliwa wakati wa kupata maji lakini kwa idadi kubwa ya ndege wanaozunguka katika makundi mbuai wanapata shida kuchagua ndege lengo na huenda wameonekana kabla hawajaweza kufika karibu na kundi. Uchaguzi wa mahali pa maji huathiriwa na topografia ya ardhi ya karibu. Firigogo huwa na kuepuka mahali palipo na kikingio kwa mbuai aina ya mamalia na hatari yao kubwa mara nyingi hutokea kwa ndege mbuai. Firigogo husafiri makumi ya kilomita mpaka madimbwi yao ya maji ya jadi na huwa na kupuuza vyanzo vya maji vya muda ambavyo vinaweza kuonekana mara kwa mara. Labda hii ina thamani ya kuokoka kwa sababu chanzo cha maji kilichokauka katika eneo kame kinaweza kusababisha mpweo na kifo. Firigogo wa Burchell katika Jangwa la Kalahari wakati mwingine husafiri zaidi ya kilomita 160 kila siku ili kufikia chanzo cha maji. Sio spishi zote zinazohitaji kunywa kila siku, na firigogo wa Tibet hana haja ya kusafiri ili kunywa kwa sababu ya wingi wa maji kutoka kwenye nyanja za theluji inayoyeyuka katika mazingira yake.

Mtago na uatamiaji

[hariri | hariri chanzo]

Firigogo wana mwenzi mmoja tu. Majira ya kuzaliana mara nyingi yanasadifu na mazao ya mbegu baada ya majira ya mvua na wakati huu makundi ya kujilisha huwa na kuvunjika katika jozi. Tago ni kishimo cha kina kifupi kwenye ardhi, wakati mwingine limewekewa vipande vichache vya majani makavu. Kwa kawaida jike huyataga mayai matatu yaliyo na rangi za kujificha, ingawa mara kwa mara kuna mayai mawili au manne. Kazi ya kuatamia inashirikiwa na katika spishi nyingi dume huatamia usiku wakati jike hukaa kwenye mayai wakati wa mchana. Mara nyingi mayai huanguliwa baada ya siku 20-25. Makinda, wanaotembea sasa hivi, wanafunikwa kwa malaika na kuondoka kiota mara tu wakati yule mwisho wa waliotoka amekauka. Wazazi hawawapatii chakula na wanajifunza, kwa mwongozo wa wazazi, nini kinacholika na kile ambacho sio. Makinda hupata maji yao kutoka malaika yaliyolowa kwenye kidari cha wapevu. Kwanza makinda ni wadogo na wachanga sana ili kudhibiti joto la mwili na hupatiwa na kivuli wakati wa sehemu ya moto kubwa ya mchana na kukingwa usiku. Wanakaa pamoja na wazazi wao, kama kikundi cha familia, kwa miezi kadhaa.

Spishi za Afrika

[hariri | hariri chanzo]

Spishi za mabara mengine

[hariri | hariri chanzo]