[go: up one dir, main page]

Nenda kwa yaliyomo

Graca Machel

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
Graça Machel mwaka 1984 pamoja na wahusika wa mapatano ya Nkomati yaani mapatano ya amani kati ya Afrika Kusini na Msumbiji ambao ni Rais Samora Machel wa Msumbiji, Rais P W Botha na Waziri Pik Botha wa Afrika Kusini

Graça Simbine Machel alikuwa mke wa marehemu Rais wa Msumbiji Samora Machel na tangu 1998 mke wa Nelson Mandela.

Alizaliwa tarehe 17 Oktoba 1946 nchini Msumbiji. Akiwa ni mtoto wa mwisho kati ya watoto sita wa mzee Simbine na bibi Nelly. Baba yake alifariki majuma matatu baada ya Graça kuzaliwa.

Graça alianza kujihusisha na siasa baada ya kwenda masomoni Lisbon, Ureno. Akiwa Lisbon alikutana na watu wengi wenye fikra za kimapinduzi waliokuwa wakijihusisha na harakati za ukombozi wa Msumbiji kupitia chama cha FRELIMO. Serikali ya Msumbiji ilipopata taarifa za kujiunga kwake kwa siri na FRELIMO ilijiandaa kumtia jela mara tu atakaporudi nchini Msumbiji. Graça alipopata habari hizo alikimbilia nchini Uswisi. Mwaka 1973 akiwa bado Ulaya aliamua kujihusisha wazi wazi na harakati za ukombozi za FRELIMO. Chama cha FRELIMO kilikuwa na shule za sekondari katika nchi mbalimbali za Afrika zilizokuwa zikitoa elimu kwa wananchama wa chama hicho. Mwaka 1974 chama hicho kilimpeleka nchini Tanzania kuwa mwalimu wa shule ya sekondari ya FRELIMO iliyoko Bagamoyo.

Akiwa Tanzania alijifunza mafunzo ya kijeshi ya kujilinda na ni katika kipindi hiki ndipo alipoweza kukutana na Samora Machelambaye alikuja kuwa mume wake na pia rais wa Msumbiji. Walifunga ndoa mwaka 1975 baada ya Msumbiji kupata uhuru wake toka kwa Wareno. Waliishi kama mume na mke hadi pale Samora Machel alipofariki kutokana na ajali ya ndege inayosadikiwa kuwa ilitunguliwa na makaburu wa Afika Kusini mwaka 1989. Kwa miaka mitano mfululizo tangu Samora Macheli afariki, Graça alivaa nguo nyeusi peke yake. Na ilipofika mwaka 1989 alistaafu wadhifa wake wa uwaziri na kujishughulisha na shughuli za maendeleo ya jamii hasa hasa watoto.

Mwaka 1998 Graça alifunga pingu za maisha kwa mara ya pili na rais wa kwanza wa Afrika Kusini huru, Nelson Mandela.