[go: up one dir, main page]

Nenda kwa yaliyomo

Bara la Antaktiki

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
Pitio kulingana na tarehe 13:34, 9 Machi 2016 na Kipala (majadiliano | michango)
Antaktiki (kijani) katika ramani ya dunia.
Antaktiki kutoka angani.
Kituo cha kisayansi katika Antaktiki.

Antaktiki ni bara lililopo kwenye ncha ya kusini ya dunia.

Jina "Antaktiki" linatokana na lugha ya Kigiriki likimaanisha "kinyume cha Aktiki", ambapo Aktiki ni eneo karibu na ncha ya kaskazini.

Bara hili lina eneo la kilomita za mraba milioni 14 na eneo hili limefunikwa karibu kabisa, yaani kwa asilimia 98% za eneo na theluji na barafu.

Kwa sababu ya baridi kali katika bara hilo, ni bara pekee ambako binadamu hawaishi kwa namna ya kudumu, isipokuwa kuna watu 5,000, hasa wanasayansi, wanaokaa kwa muda katika vituo vyao.

Uvumbuzi

Bara la Antaktiki haikujulikana hadi karne ya 19 lakini wataalamu wa jiografia waliwahi kuhisi tangu zama za kale ya kwamba eneo kubwa la nchi kavu liko kwenye sehemu ya kusini ya dunia[1]. Tangu Aristoteli wataalamu waliamini ya kwamba dunia ilipaswa kuwa na uwiano fulani hivyo kuwepo kwa bara kubwa ingekuwa lazima kuingana na mabara ya nusutufe ya kaskazini. Nchi hii isiyojulikana kwa muda mrefu ukaitwa kwa jina la Kilatini "terra australis" yaani "nchi ya kusini" na pia kuchorwa kwenye ramani za dunia zilizoanza kutengenezwa tangu safari za wavumbuzi Wareno waliozunguka dunia mara ya kwanza. Ila tu ramani hizi za kwanza zilikuwa njozi tu.

Kundi la kwanza wa kufika kusini kwa kutosha na kuona kona ya barafu ya Antaktiki lilikuwa mwaka 1820 msafara wa kisayansi wa nahodha Fabian von Bellingshausen (Mjerumani Baltiki katika utumishi wa Tsar wa Urusi) akifuatwa mwaka uleule na nahodha Edward Bransfield wa Uingereza na tena Mmarikani Nathaniel Palmer. Ila tu hakuna uhakika kama wavumbuzi hao walitambua tayari ya kwamba waliona bara jipya[2].

Pamoja na taarifa za mabaharia wengine waliopita kwenye pwani bado haikueleweka kama hapa karibu na ncha ya kusini kulikuwa na visiwa mbalimbali au nchi kavu zaidi. Ni misafara ya Wafaransa na Wamarekani mnamo mwaka 1840 iliyoweza kuthebitisha ya kwamba ncha ya kusini ilipatikana ndani ya bara jipya. Sasa shauku ya upelelezi ilififia kwa sababu haikueleweka kuna nini katika bara jipya.

Tangu mwaka 1890 Shirika la Kifalme la Jiografia (Royal Geographic Society) nchini Uingereza lilianza upya kusisitiza umuhimu wa utafiti wa Antaktiki iliyokuwa sehemu ya mwisho wa dunia isiyochunguliwa bado kabisa. Misafara mbalimbali kutoka nchi tofauti ilifuatana sasa na kupeleleza Antaktiki:

  • 1907 ncha sumaku ya kusini ilifikiwa na msafara wa Mwingereza Ernest Shackleton
  • 1910 misafara miwili kutoka Norwei na Uingereza ilishindana kufika ncha ya kusini ya kijiografia. Mnorwei Roald Amundsen alikuwa wa kwanza kufika nchani tarehe 14 Disemba 1910 akarudi salama kwa meli yake. Kundi la Mwingereza Robert Scott likachelewa siku 33 likakuta bendera ya Norwei na hema ya Amundsen. Kwenye njia ya kurudi Scott alipata hali ya hewa mbaya akaishia chakula chote akafa pamoja na wenzake katika barafu.

Katika miaka iliyofuata idadi ya misafara iliongezeka. Tangu 1929 eropleni zilitumika pia katika upelelezi. Ni hasa Mmarekani Richard Byrd aliyeongoza misafara kadhaa akitumia ndege akaweza kuweka msingi kwa ramani kamili ya Antaktiki.

Jiografia

Ramani ya Antaktiki

Nchi ya bara la Antaktiki ina takriban umbo la duara isiyo kamili ikizunguka ncha ya kusini. pande zote inapakana na bahari ni mahali ambako maji ya kusini ya Pasifiki, Atlantiki na Bahari Hindi inakutana. Kwa namna nyingine inawezekana kusema inazungukwa na Bahari ya Kusini. Eneo lake ni zaidi ya kilomita za mraba milioni 14 ni bara la tano duniani kwa ukubwa. Umbali kutoka pwani na pwani uko baina kilomita 4,500 na 5,600. [3] Pwani ina urefu wa kilomita 17,968.

Sehemu za Antaktiki

Safu ya Milima ya kuvukia Antaktiki (ing. Transantarctic Mountains) inagawa bara kwa sehemu mbili za Antaktiki Magharibi na Antaktiki Mashariki. Mpaka huu unalingana takriban na longitudo ya 180.

  • Antaktiki Magharibi ni upande ndogo zaidi. Ndani yake inagawiwa kwa rasi kadhaa kwa hiyo ina athira ya tabianchi kutoka bahari. Hata kama sehemu kubwa inafunikwa na barafu halijoto haishuki chini mno jinsi ilivyo upande wa mashariki. Rasi kubwa ni Rasi ya Antaktiki (ing. Antarctic Peninsula)
  • Antaktiki Mashariki inafana zaidi na nusutufe hakuna rasi au hori kubwa. Kwa hiyo tabianchi ni zaidi ya kibara. Uso unafunikwa na ganda la barafu lenye unene wa kilomita 1.6 au zaidi. Halijoto ya duni inayojulikana ilipimika 1983 kuwa sentigredi 89,4 chini ya sifuri.

Visiwa

Kisiwa cha Berkner jinsi inavyoonekana chini ya ngao ya barafu kwenye picha ya satelaiti

Visiwa kadhaa vinahesabiwa kuwa sehemu za Antaktiki. Sehemu ya visiwa hivi viko ndani ya maji ya bahari. Vingine inafunikwa kwa barafu ya kudumu na hivyo haionekani mara moja ya kwamba kuna kisiwa maana sehemu nyingi ngao nene la barafu ya kudumu linaingia baharini nje ya pwani.

Visiwa hivi ni pamoja na

  • Kisiwa cha Alexander ambacho ni kisiwa kikubwa cha Antaktiki; kina upana wa kilomita 200 na urefu wa kilomita 378 na eneo la 49,070 km². Kinatengwa na bara kwa mfereji wa bahari mwenye upana wa kilomita 24-60 lakini yote inafunikwa kwa barafu ya kudumu ila tu sehemu ya pwani inaiongia katika maji ya bahari
  • Kisiwa cha Berkner ambacho ni kisiwa kikubwa cha pili chenye urefu wa 320 km na upana wa 135 km na eneo la 43,873 km². Kinafunikwa kabisa na ngao ya barafu hakionekani hata kutoka baharini.
  • Visiwa vya Joinville, Roosevelt, Ross na kadhalika

Milima

Ncha za Milima ya kuvukia Antaktiki zinaonekana juu ya ngao ya barafu ya kudumu

Miilima mingi ni sehemu ya Safu ya Milima ya kuvukia Antaktiki (au: milima transaktiki) ambayo ni safu ndefu yenye urefu wa kilomita 3,500 na kifikia kimo cha mita 4500 na zaidi. Ncha za milima mirefu yake zinaonekana juu ya uso wa ngao ya barafu inayofunika bara lote. Mlima mrefu katika safu hii ni Mount Kirkpatrick yenye urefu wa mita 4528 juu ya UB.

Pale ambako Rasi ya Antaktiki inaanza kuna safu ya milima ya Ellsworth na hapa uko mlima mrefu kabisa wa bara ni Mount Vinson yenye mita 4,892 juu ya UB.

Kuna pia volkeno kadhaa, nyingine zinalala nyingine ziko hai. Volkeno hai ndefu ni Mount Erebus yenye kimo cha mita 3,794, iko kwenye kisiwa cha Ross.

Ngao ya barafu ya kudumu

Ramani inaonyesha unene na uenezi wa ngao ya barafu ya Antaktiki:
- Rangi za buluu zinaonyesha unene wa ngao ya barafu kwa kutumia hatua za mita 1,000;
- buluu-nyeupe ni ngao ya barafu inapofunika maji ya bahari
- mistari minene: miinuko inayogawa mwendo wa barafu
- mistari membamba: mielekeo ya mwendo wa barafu
- nyekundu: sehemu zisizofunikwa na barafu

Tabia ya pekee ya Antaktiki ni nago ya barafu inayofunika karibu uso wote wa nchi yake pamoja na sehemu za bahari ya karibu. Ngao ya barafu hii ni mkusanyiko mkubwa wa barafu duniani. Unene yake (yaani kimo juu ya ardhi) unafikia hadi mita 4,500.

Ngao ya barafu inajumlisha

  • asilimia 90 ya barafu yote duniani
  • asilimia 70 ya maji matamu yote duniani

Ni asilimia 2-3 za eneo lote la bara zisizofunika kwa barafu yaani 280,000 km².

Ngao hiyo ilianza kutokea miaka milioni kadhaa iliyopita. Uzito wake ni mkubwa na inaaminiwa ya kwamba bara lote lilishuka chini kiasi na kama siku moja ngao ya barafu ingepotea itapanda tena juu kwa mita kadhaa.

Barafu hii inashika maji mengi kiasi ya kwamba kama barafu yote itayeyuka siku moja uwiano wa bahari duniani kote itapanda juu takriban mita 61.

Mito, maziwa na barafuto

Ziwa la Lake Vostok - uso wa ziwa unaonekana kama eno tambarare; wakati wa joto kuna maji
Barafuto kubwa (mto wa barafu) barani Antaktiki

Tabia ya pekee ya Antaktiki ni pia uhaba wa mito. Mito yote inayotokea ni ya maji ya barafu ya kuyeyuka wakati wa "majira ya joto" katika miezi ya Februari na Machi. Katika sehemu nyingien ya mwaka mito yote inaonekana kama kanda la barafu. Mto mkubwa ni Onyx River inayofikia urefu wa kilomita 30 ukiishia katika Ziwa Vanda. Mito haina samaki lakini kuna mikrobi na algae katika mito mikubwa zaidi.

Kuna maziwa kadhaa chini ya ngao la barafu. Hata kama jotoridi yao ni chini ya sentighredi 0 badi yanaweza kuwa na maji ya kiowevu kwa sababu shinikizo kubwa ya ngao ya barafu inashusha halijoto ya kugnadisha maji hasa kama maji ni ya chumvi.

Barafu ya ngao haikai kimyakimya lakini yote ina mwendo ikifuata mtelemko wa usio wa nchi. Katika sehemu kadhaa barafu ina mwendo wa haraka zaidi na sehemu hizi zinaitwa "mito ya barafu" na ni aina ya barafuto. Mito ya barafu hii iko yenye urefu hadi kilomita mamia na upana wa 50 km na unene wa kilomita 2. Mwendo unafikia hadi mita 1.000 kwa mwaka. Pale inafikia kwenye ufuko wa bahari inajenga ulimi ya barafu inayosukumwa katika maji.


Hali ya Kisiasa

Madai ya mataifa katika Antaktiki

Antaktiki si nchi wala dola na hakuna wenyeji au wananachi. Lakini madola mbalimbali yalitangaza madai ya kutawala sehemu za eneo lake. Madai haya hayalingani na mara kadhaa kuna mataifa mbalimbali yanayodai sehmu ileile.

Mataifa yanayodai kutawala sehemu za Antaktiki ni pamoja na Argentina, Australia, Chile, Ufaransa, New Zealand, Norwei na Ufalme wa Maungano.

Tangu 1961 kuna Mkataba wa Kimataifa kuhusu Antaktiki unaosimamisha madai yote ya utawala bila kuyafuta. Mataifa yote yana haki ya kuwa na vituo vya kisayansi. Mapatanao ya kando yaliweka masharti makali kwa shughuli za kiuchumi na hado sasa imewezekana kuzuia migodi na uchimbaji wa madini.

Mengineyo

Mtoto wa kwanza kuzaliwa barani huko alizaliwa mwaka 1984. Kwa sasa kuna shule kadhaa na kanisa moja.

Eneo lake ni kubwa kushinda Ulaya lakini hakuna mti hata mmoja. Bara hili linajulikana kama jangwa baridi.

Bara liko kati ya bahari za Pasifiki, Atlantiki na Bahari Hindi.

Kuna volkeno hai moja inayotema moto baraniː ni mlima wa Mount Erebus.

Marejeo

  1. [Aristoteli (mwaka 350 [KK]) katika fungu la tano la kitabu chake juu ya metrolojia]: "kuna kanda mbili zinazoweza kukaliwa na watu duniani: moja kwa upande wa juu, au karibu na ncha yetu ya kaskazini, nyingine karibu na ncha nyingine, au ncha ya kusini"
  2. Terence Armstrong, Bellingshausen and the discovery of Antarctica, Polar Record / Volume 15 / Issue 99 / September 1971, pp 887-889
  3. ilhali ncha ya kusini iko takriban katikati ya bara, kila upande kutoka hapa uko kaskazini.

Viungo vya nje