[go: up one dir, main page]

Petro wa Alkantara

(Elekezwa kutoka Petro wa Alcantara)

Petro wa Alkantara, ambaye awali aliitwa Juan Garavita (Alcántara, Hispania 1499 - Arenas, Estremadura, 18 Oktoba 1562), alikuwa padri wa Kanisa Katoliki na mtawa wa shirika la Ndugu Wadogo.

Livio Mehus, Mtakatifu Petro wa Alkantara akimkomunisha mtakatifu Teresa wa Avila; picha ya mwaka (1683) inayotunzwa Prato (Italia).

Alikuwa maarufu kwa kipaji cha shauri na kwa ugumu wa maisha yake ya toba; hivyo alifufua uaminifu kwa kanuni katika konventi za shirika lake huko Hispania, mbali ya kumsaidia Teresa wa Yesu kurekebisha lile la Wakarmeli[1].

Anaheshimiwa na Wakatoliki kama mtakatifu.

Sikukuu yake inaadhimishwa kila tarehe 18 Oktoba[2].

Maisha

hariri

Baba yake, Petro Garavita, alikuwa gavana wa mkoa, na mama yake alikuwa wa ukoo bora wa akina Sanabia. Kisha kusoma lugha na falsafa mjini kwake, alipokuwa na umri wa miaka 14 alipelekwa kusoma chuo kikuu cha Salamanca.

Alipomaliza, mwaka 1515 alijiunga na Wafransisko wa konventi ya urekebisho huko Manxaretes, na alipofikia miaka 22 alitumwa kuanzisha nyingine huko Badajoz.

Kisha kupata upadirisho mwaka 1524 mwaka uliofuata alichaguliwa guardiano (kiongozi wa jumuia) ya Robredillo.

Alipata sifa kama mhubiri: hotuba zake, zilizofuata hasa Biblia, zililenga watu duni zaidi.

Kisha kuchaguliwa mtumishi wa kanda ya Mt. Gabrieli mwaka 1538, Petro alitunga katiba kali akaipendekeza kwenye mkutano wa kanda huko Plasencia mwaka 1540, lakini alikataliwa. Hapo akajiuzulu akaenda na Yohane wa Avila kwenye milima ya Arabida (Ureno), akajiunga na padri Martino wa Santa Maria kuishi upwekeni.

Baada ya ndugu wengine kujiunga nao, jumuia nyingi ndogondogo zilianzishwa. Petro akachaguliwa kuwa guardiano na mlezi wa wanovisi huko Pallais. Mwaka 1560 jumuia hizo ziliunda kanda ya Arabida.

Aliporudi Hispania mwaka 1553, aliishi upwekeni zaidi ya miaka miwili, halafu akaenda miguu mitupu hadi Roma akakubaliwa na Papa Julio III aanzishe konventi fukara kadhaa chini ya mamlaka ya mkuu wa Wakonventuali.

Mwaka 1556 konventi hizo ziliunda kanda ndogo chini ya Petro; halafu mwaka 1561 kanda kamili, jina lake Mt. Yosefu.

Bila ya kujali upinzani uliompata awali, alitunga katiba kali zaidi iliyoongoza urekebisho huo mpya ulioenea haraka Hispania na Ureno.

Mwaka 1562 kanda hiyo ilihamishwa chini ya mamlaka ya mkuu wa Waoservanti.

Mafungamano

hariri

Kati ya watu waliompenda kuna watakatifu Fransisko Borgia, Yohane wa Avila na Teresa wa Yesu. Barua ya Petro kwa bikira huyo ya tarehe 14 Aprili 1562 ndiyo iliyomtia moyo wa kuanzisha monasteri ya kwanza ya urekebisho wa Wakarmeli Peku huko Avila tarehe 24 Agosti mwaka huohuo.

Kitabu cha Teresa juu ya Maisha yake mwenyewe kina habari nyingi kuhusu Petro na karama zake. Mwenyewe anashuhudia kwamba alimtokea mara baada ya kufa na kumuambia, "Heri toba iliyonipatia utukufu mkubwa namna hii".

Maandishi

hariri

Zaidi ya Katiba na barua nyingi kuhusu maisha ya kiroho, aliandika Kitabu juu ya sala, kilichoenea na kutafsiriwa katika lugha mbalimbali.

Heshima baada ya kifo

hariri

Alitangazwa mwenye heri na Papa Gregori XV tarehe 18 Aprili 1622; na mtakatifu na Papa Klementi IX tarehe 28 Aprili 1669.

Kutokana na urekebisho wa kitawa alioushughulikia lilitokana tawi la Pekupeku. Pia alichangia urekebisho wa Wakarmeli ulioanzishwa na Teresa wa Yesu: ndiyo sababu katika Basilika la Mt. Petro huko Vatikani sanamu yake inashika nafasi kati ya waanzilishi muhimu zaidi wa historia ya Kanisa.

Tazama pia

hariri

Tanbihi

hariri

Viungo vya nje

hariri
  Makala hii bado ni mbegu.
Je, unajua kitu kuhusu Mkristo huyu, kama wasifu wake, habari za maisha au kazi yake?
Je, unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuiongezea habari.