[go: up one dir, main page]

Joseph Vissarionovich Stalin (kwa Kirusi: Иосиф Виссарионович Сталин, Iosif Vissarionovich Stalin; jina la kiraia: Джугашвили, Dzhugashvili, kwa Kigeorgia: იოსებ ჯუღაშვილი, Ioseb Jughashvili; 18 Desemba (katika Kalenda ya Juliasi: 6 Desemba) 18785 Machi 1953) alikuwa mwanasiasa wa Urusi kutoka Georgia aliyeshiriki pamoja na Lenin katika Mapinduzi ya Urusi ya 1917[1] na kuwa kiongozi wa chama cha kikomunisti na hivyo kiongozi mkuu wa Umoja wa Kisovyeti baada ya kifo cha Lenin[2].

Josef Stalin mwaka 1942.

Alitawala Urusi kama dikteta kwa unyama na kusababisha vifo vya mamilioni ya watu. Vifo vingi vilisababishwa na kufuta mali ya wakulima na kuwalazimisha kulima kama makundi, iliyosababisha njaa na kuua watu milioni 6 au zaidi.[3] Mnamo 1935 Stalin aliagiza katiba mpya iliyoweka mamlaka yote mkononi mwa Kamati Kuu (politbureau) ya chama alichoongoza. Pamoja na mabadiliko hayo alianza kempeni za "kusafisha" chama. Kuanzia mwaka 1935 raia elfu nyingi, pamoja na wanachama wa chama cha Kikomunisti na hata wajumbe wa Halmashauri Kuu (Central Committee) walikamatwa; wakibahatika waliamriwa kuhamia mji katika sehemu mbali na Moscow; wengine walihukumiwa na maelfu kuuawa. Katika kipindi cha "utakaso mkuu" viuongozi wengi wa zamani pamoja na viongozi wengi wa jeshi waliuawa. Katika kipindi hiki, takriban milioni 1.6 walikamatwa, watu 700,000 walipigwa risasi na idadi isiyojulikana ilikufa kutokana na mateso katika magereza ya polisi ya siri.[4]

Stalin alifaulu kujenga uchumi wa viwanda na kutetea nchi dhidi ya mashambulio ya Ujerumani wakati wa Vita Kuu ya Pili ya Dunia. Alikuwa kati ya washindi wa Vita Kuu ya Pili akapanua utawala wake juu ya nchi za Ulaya ya Mashariki na ya Kati kama vile Poland, Ucheki, Hungaria, Romania, Bulgaria na sehemu ya mashariki ya Ujerumani. Nchi hizi zote zlilazimishwa kukubali utawala wa vyama wa kikomunisti na kuendelea kwa mfumo wa kidikteta.

Stalin alikubaliwa kama kiongozi wa nchi zote za kikomunisti pamoja na China, Vietnam na Korea ya Kaskazini hadi kifo chake.

Stalin alikufa baada ya mshtuko wa ubongo; alikutwa kwenye nyumba yake tarehe 1 Machi 1953 akilala chini na kushindwa kuongea. Lavrentiy Beria, mkuu wa ujasusi na mwanachama wa Kamati Kuu ya Chama alidai baadaye kwamba alimsumisha Stalin[5].

Alifuatwa na Nikita Krushchov kama kiongozi wa chama na Umoja wa Kisovyeti.

Joseph Stalin alikuwa na wake wawili kwa vipindi tofauti: mke wa kwanza aliitwa Ekaterine Svanidize (1906-1907), na wa pili aliitwa Nadezhda Alliluyeva (1919-1932). Pia alikuwa na watoto watatu walioitwa Yakov Dzhugashvilli, Vasily Dzhugashvilli na Svetlana Alliluyeva.

Jina la utani la Joseph Stalin lilikuwa ni 'Koba'.

Marejeo

  1. Conquest, Robert (1991). Stalin: Breaker of Nations. New York and London: Penguin. ISBN 978-0-14-016953-9, uk 64
  2. Service, Robert (2004). Stalin: A Biography. London: Macmillan. ISBN 978-0-333-72627-3, uk 276
  3. Khlevniuk, Oleg V. (2015). Stalin: New Biography of a Dictator. Translated by Nora Seligman Favorov. New Haven and London: Yale University Press. ISBN 978-0-300-16388-9, uk 110-111, 116
  4. Khlevniuk 2015, uk 151
  5. Felix Chuev: Molotov Remembers: Inside Kremlin Politics. Ed. Albert Resis. Ivan R. Dee, Chicago 1993, ISBN 1-56663-027-4, uk
  Makala hii kuhusu mwanasiasa fulani bado ni mbegu.
Je, unajua kitu kuhusu Josef Stalin kama wasifu wake, habari za maisha au kazi yake?
Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari.